Mama alipokufa kitu nilirithi kutoka kwake ni kitanda na deni la kodi ya nyumba - Boniface Mwangi

“Mamangu alifariki nikiwa na umri wa miaka 17 na nikabaki peke yangu duniani. Babangu ni deadbeat Kwa sababu wakati nilikuwa nazaliwa tayari walikuwa wametengana na mamangu,”

Muhtasari

• Akiwa mitaani, alifanya kazi zisizo rasmi kama kuchuuza vitabu, midoli, maua na vitu vingine vidogo vidogo.

• Mwangi alimsifia mamake akisema kwamba alikuwa mzazi aliyemtakia mwanawe kila kitu kizuri maishani na kwamba hakuwa anamsumbua wakati anasoma.

Boniface Mwangi.
Boniface Mwangi.
Image: Facebook

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi amefunguka jinsi alipitia maisha magumu baada ya kutoroka nyumbani na kisha baadae kufungwa katika jela ya watoto akihudhuria masomo kwenye shule ya kurekebisha tabia.

Katika maongezi na Obinna, Mwangi alisema kwamba baadae alifukuzwa kutoka kwa shule ya marekebisho ya tabia kwa watoto waliofungwa jela na kulazimika kutafunga maisha mitaani.

Akiwa mitaani, alifanya kazi zisizo rasmi kama kuchuuza vitabu, midoli, maua na vitu vingine vidogo vidogo.

Mwangi alisema alilazimika kuzamia kazi hizi kwani hakuweza kuhudhuria masomo ya shule ya upili baada ya kufukuzwa katika shule ya marekebisho ya tabia akiwa na umri wa miaka 14.

Cha kushangaza Zaidi, mwanaharakati huyo alisimulia kwamba akichuuza vitabu mitaani, alikuwa anaishi na mama yake na baadae alipata pigo kubwa kwa kufiwa na mama mzazi.

Mwangi alisema kwamba mama yake alipofarii, alibaki na urithi wa madeni ya nyumba yenye chumba kimoja cha kukodisha pamoja na kitanda kidogo.

“Nilichuuza vitabu katika mitaa na barabara hapa Nairobi, midoli, maua… unajua kusema ukweli wakati mama yangu alipofariki, kitu pekee nilichokirithi kutoka kwake ni kitanda cha shilingi 600 kwenye nyumba ya chumba kimoja na rundo la madeni ya kodi ya nyumba. Na hapo nilibaki kujitegemea mwenyewe,” Mwangi alisema kwa sauti ya huruma.

Hata hivyo, Mwangi alibainisha kwamba si yeye mzawa pekee kwa mama yake bali wako ndugu 7, mmoja alifariki kwa hiyo wako sita kwa sasa.

“Mamangu alifariki nikiwa na umri wa miaka 17 na nikabaki peke yangu duniani. Babangu ni deadbeat na yuko mahali tu sijui. Kwa sababu wakati nilikuwa nazaliwa tayari walikuwa wametengana na mamangu,” alisema.

Mwangi alimsifia mamake akisema kwamba alikuwa mzazi aliyemtakia mwanawe kila kitu kizuri maishani na kwamba hakuwa anamsumbua wakati anasoma.

Lakini baada ya kifo chake, alilazimika kuhudhuria masomo ya Biblia, akawa mhubiri kwa vijana kabla ya kujiunga na chuo anuwai cha uanahabari wa kupiga picha baadae katika umri wake wa miaka ya 20s.