Msanii wa kizazi kipya nchini Tanzania Diamond Platnumz amevunja kimya chake kuhusu sababu za kufanya ngoma kwa mara ya pili tena chini ya miaka mitatu na msanii wa Rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide.
Kupitia Instagram, Diamond aliandika ujumbe wa kihisia kumhusu mkongwe huyo wa muziki wa Kongo akisema kwamba ni mtu ambaye amekuwa akimpa hamasa ya kutaka kufanya vizuri katika muziki lakini pia kudumu katika ngazi za juu kwa muda mrefu.
Diamond alisema haya baada ya kolabo yao mpya – Achii – kuweka rekodi ya kufikisha watazamaji milioni moja ndani ya saa 21 na kusema kwamba yeye ni hsabiki mkubwa wa Koffi tangu akiwa mdogo.
Msanii huyo alifichua kwamba Olomide ni msanii ambaye anajitolea sana katika kazi anayoifanya hivyo kuleta faraja na ufanisi mkubwa katika mradi wowote anaoufanya haswa kwa kuwainua wasanii wachanga.
“Toka nikiwa mdogo na Famila yetu nyumbani Nimekua nikitazama Miziki ya @koffiolomide_officiel na kuwa moja ya Shabiki zake wakubwa… na ndiomaana siku zote imekua ni faraja kufanya nae wimbo pamoja.. Namshukuru kwa namna ya mara zote anavyojitoa Asilimia mia kuhakikisha tunapata wimbo ambao utawapa Raha Mashabiki zetu… Na Hii hapa kazi yetu mpya inaitwa #Achii” Diamond alisema.
WImbo huo mpya umetoka siku mbili zilizopita jambo ulishindwa kufikia rekodi iliyowekwa na ule wa Waah wa mwaka 2020, bado unazidi kujikokota kwa kasi nzuri.
Hata hivyo, baadhi ya washikadau wa muziki walihisi kwamba walikuwa wanategemea kitu chenye ladha tofauti kutoka kwa wasanii hao wawili lakini wakapata ladha ya wimbo wa Achii kwa ukarimu inafanana ile ya wimbo wa Waah, kutoka kwa midundo hadi kwenye staili za kusakata densi.