Kabla ya Willis Raburu, mimi ndio nilikuwa mwanzilishi wa shoo ya 10/10 - 2Mbili afichua

"Mimi ndio nilikuwa mmoja wa waanzilishi wa shoo ya 10 over 10 kabla hata haijaanza kwenda hewani. Mimi JB Masanduku na Fish ndio tuliianzisha mwaka 2016." - 2Mbili.

Muhtasari

• Mchekeshaji huyo ambaye pia ni mkuza maudhui alisema hata hivyo kwamba anawaamini na uwakubali walioteuliwa.

2Mbili asema ndio alianzisha 10Over10
2Mbili asema ndio alianzisha 10Over10
Image: Facebook

Mchekeshaji 2Mbili amefichua ukweli ambao wengi hawakuwa wanajua kuhusu shoo ya vijana kwenye runinga ya Citizen, 10 over 10.

Katika mahojiano na SPM Buzz, 2Mbili alifunguka sababu yake ya kutoitwa kwenda kufanya usaili wa kuvivaa viatu vikubwa vilivyoachwa na aliyekuwa mwongozaji wa kipindi hicho Willis Raburu.

2Mbili alikiri kwamba kweli hakuitwa kwenda kufanya usaili lakini akafichua kwamba wasichojua wengi ni kwamba yeye ndiye alikuwa mwanzilishi wa shoo hiyo kabla hata Willis Raburu kuikabidhiwa.

“Ambacho watu hawajui ni kwamba mimi ndio nilikuwa mmoja wa waanzilishi wa shoo ya 10 over 10 kabla hata haijaanza kwenda hewani. Mimi JB Masanduku na Fish ndio tuliianzisha mwaka 2016. Tulialikwa Royal Media na sisi ndio tulianzisha kabla hata ujio wa Willis Raburu,” 2Mbili alisema.

Akizungumzia ilikuwaje mpaka hawakuendelea kuiongoza shoo hiyo na badala yake ikapewa kwa Willis Raburu, 2Mbili alisema;

“Tuliambiwa tungoje kodogo kidogo tukamuona Willis Raburu akiongoza shoo hiyo. Lakini bado mimi najivunia kwa sababu nimewahi kuwa mmoja wa hiyo shoo ikiwa ni ya awali kabisa,” alisema.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni mkuza maudhui alisema hata hivyo kwamba anawaamini na uwakubali walioteuliwa ili kuwania nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Raburu mwezi mmoja uliopita.

“Lakini bado orodha ya wale walioitwa pale mimi badi nawaaminia wanaweza. Mimi sijaona mtu yeyote pale ambaye naweza sema kwamba naweza bishana na yeye. Nimeona kina Obinna, Kamene na wengine lakini namkubali Gudah Man,” 2Mbili alisema.