Mpishi Maliha amekanusha vikali madai ya 2Mbili kwamba maceleb walimaliza chakula

Mpishi huyo alifichua kwamba chakula alichokipika takribani asilimia 40 kilitokana na michango na watu huku yeye akiingia mfukoni mwake kwa asilimia 60.

Muhtasari

• “Naweza kuwaambia kwamba fanya mazoezi, lazima mtu anayepaga kwenda kufanya kitu, usiingie kichwa kichwa" - alishauri.

Chef Maliha na 2Mbi;i
Chef Maliha na 2Mbi;i
Image: Instagram

Mpishi Maliha Mohammed amekanusha vikali kauli ya mchekeshaji 2Mbili kwamba watu mashuhuri waliojitokeza kwenye hafla yake ya kukimbizana na rekodi ya dunia ya Guiness walikwenda tu kwa ajili ya kula chakula.

Akizungumza na mwandishi wa Radio Jambo Moses Sagwe, Maliha alisema kwamba watu mashuhuri waliojitokeza kwenye jiko lake wakiwemo wanasiasa, wanablogu na maceleb wengine wengi hawakwenda kule mahsusi kwa ajili ya mlo.

Badala yake, Maliha alisema kwamba idadi kubwa ya watu maarufu waliofika kwenye shinano lake walimpelekea misaada ikiwemo ya kifedha, chakula na wengine kujumuika naye ili kushuhudia akiandikisha historia ya kupika ndani ya nyumba kwa Zaidi ya saa 90 bila kukoma.

Alikanusha kauli hiyo iliyotolewa na 2Mbili kwenye Instastory yake mwanzoni mwa wiki jana wakati alikuwa akimhongera kwa kuweka rekodi akisema kwamba kwa bahati mbaya wengi walijitokeza kwa ajili ya msosi.

“Hapana kwa kweli, mimi siwezi kuwahukumu watu. Watu walikuja nikafurahi, walikuja kuniona na kunipa sapoti, kifedha, kijamii nilifurahi ujio wao, angalau walijitokeza. Walitenga muda wao wakaja sio kama wengine ambao hawakuja walijiweka kando, hawanitambui nafanya nini. Mimi ninashukuru sana walikuja na chakula kilikuwa cha kutosha. Niliwapikia chakula watu wakala, tukaenda kwa kituo cha Watoto mayatima pia tukashiriki…” alisema.

Mpishi huyo alifichua kwamba chakula alichokipika takribani asilimia 40 kilitokana na michango na watu huku yeye akiingia mfukoni mwake kwa asilimia 60.

“Nilikuwa na ufadhili kutoka kwa makampuni kadhaa, kuna watu walikuja kunipa msaada angalau kwa asilimia 40, hiyo ingine ilitoka kwa mfuko wangu,” alisema.

Maliha alisema kwamba azma yake kuu katika upishi ni kuendelea kuvunja rekodi lakini pia kuendeleza academia yake ya kuwafunza watu jinsi ya kupika vyakula haswa vya kiafrika.

Alisema kuwa haoni ubaya kwa Wakenya wengine wanaojitokeza kutoa chagamoto kwa rekodi zake lakiji alikuwa na ushauri mmoja kwa wanapanga kuingia kwenye uwanja wa kuvunja rekodi ya Guiness.

“Naweza kuwaambia kwamba fanya mazoezi, lazima mtu anayepaga kwenda kufanya kitu, usiingie kichwa kichwa, fanya utafiti, fanya mazoezi kwa sana hadi pale unahisi kabisa kwamba uko tayari, usitake watu wakusukume, fanya wakati unahisi uko tayari kabisa,” Maliha alisema.