Tanzania Rapa pekee anaweza nishinda ni Professor Jay - Stevo Simple Boy

"Hata kama OG hajamaliza hiyo bifu, basi mimi nitaingilia niende mpaka pale Tanzania niwabwage hao marapa wote watukome. Mimi naingia kama amiri jeshi mkuu." Stevo alisema.

Muhtasari

• "Hawa wengine ni bure tu. Rosa Ree bado ni mdogo sana na haniwezi,” Stevo Simple Boy alisema.

• Stevo alisema kuwa ana mpango wa kufunga safari kwenda Tanzania ili kuwaonesha kivumbi marapa wa huko ili kujizolea heshima.

Stevo atangaza vita dhidi ya Tanzania
Stevo atangaza vita dhidi ya Tanzania
Image: Screengrab

Rapa wa Kenya Stevo Simple Boy amekumbatia mzozo wa vita vya maneno baina ya Sanaa ya Hip Hop ya Kenya na ile ya nchi jirani ya Tanzania.

Katika mahojiano na wanablogu wa habari za mitandaoni, Stevo alisema kwamba rap ya Tanzania haina mashiko hata kidogo kwani wao hurap kwa lugha ya Kiswahili ambayo haivuki kupita Mlima Kilimanjaro.

 Stevo alisema kuwa nchini yeye na Khaligraph Jones ndio wafale pekee wa muziki huo wa rap akisema kuwa katika Sanaa ya rap ya Tanzania, haoni msanii yeyote ambaye anaweza kumkalisha kitako.

Stevo alisema mkongwe Professor Jay ndiye msanii peke anayeweza kumtingisha kidogo tu lakini wengine akawataja kama baridi ya msimu tu inayopita.

“Hamna msanii wa rap hata mmoja anayeweza nitoa kwenye ulingo. Labda tu mtu mmoja tu ndio anaweza nitoa. Mkongwe Professor Jay pekee yake. Hawa wengine ni bure tu. Rosa Ree bado ni mdogo sana na haniwezi,” Stevo Simple Boy alisema.

Stevo aliwahimiza wasanii marapa wa Kenya kujitosa kabisa kwenye ulingo wa kupambana kimaneno katika rap battle akisema kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuiheshimisha Sanaa ya Kenya haswa kwenye kitengo cha rap.

Stevo alisema kuwa ana mpango wa kufunga safari kwenda Tanzania ili kuwaonesha kivumbi marapa wa huko ili kujizolea heshima.

“Watu walikuwa wanasema Stevo Simple Boy aingilie kati. Sasa natangaza pia mimi nimeingilia rasmi. Hata kama OG hajamaliza hiyo bifu, basi mimi nitaingilia niende mpaka pale Tanzania niwabwage hao marapa wote watukome. Mimi naingia kama amiri jeshi mkuu. Sisi tunaangalia ubabe wa Tanzania na Kenya, ni nchi gani ina marapa ambao wana uwezo mkubwa wa kuchana,” alisema.

Khaligraph Jones ndiye alikiwasha wiki jana akiwapa changamoto marapa wa Tanzania na kusema kuwa yeyote anayejiona kama anamuweza basi amekaribishwa kwenye ulingo ili wachuane kwenye kutema madini yenye vina.