Rayvanny avutiwa na Zuchu, ahofia kupiga hatua kwa kumuogopa Diamond (+video)

Rayvanny alikiri kuwa alitamani kwenda kutingiziwa kiuno na Zuchu lakini akahofia kuingia kwenye matatizo na Diamond.

Muhtasari

•Mara baada ya kupanda jukwaani, Zuchu alisimama kando ya Rayvanny, akainama na kuanza kutikisa kiuno chake kwa mtindo wa kuvutia.

•Rayvanny pia hakukosa kumshambulia mwanablogu wa Tanzania Mange Kimambi ambaye hivi majuzi amehusika kwenye mgogoro na Zuchu.

Rayvanny na Zuchu
Image: HISANI

Mastaa maarufu wa Bongo, Rayvanny na Zuchu walishiriki jukwaa moja wikendi wakati wa Tamasha la Wasafi Festival 2023 mjini Mtwara, Tanzania.

Zuchu aliungana na bosi huyo wa Next Level Music jukwaani alipokuwa akiimba kolabo yao maarufu ‘Number One’ ambayo waliimba takriban miaka mitatu iliyopita.

Mara baada ya kupanda jukwaani, binti huyo wa Khadija Kopa alisimama kando ya Rayvanny, akainama na kuanza kutikisa kiuno chake kwa mtindo wa kuvutia.

Baada ya kuona hivyo, bosi huyo wa NLM alipata ubunifu na kupindisha maneno ya wimbo aliokuwa akiimba na kuweka maneno mengine akikiri kuwa alitamani kwenda kutingiziwa kiuno na Zuchu lakini akahofia kuingia kwenye matatizo na aliyekuwa bosi wake, Diamond Platnumz.

“Penzi limetaradadi, napepewa. Harufu ya marashi rashi. Nikitouch gusa shingoni. Hii! Uvae baibui kanga. Viatu vya kuchuchumia kangaroo.. ningekuja kwa nyuma, ila Simba atakuja nivunja miguu,” Rayvanny aliimba.

Rayvanny pia hakukosa kumshambulia mwanablogu wa Tanzania Mange Kimambi ambaye hivi majuzi amehusika kwenye mgogoro na Zuchu.

“Ukizungushia shanga, inashuka inapanda chini juu... Mimi nitakusifia, sikutukani kama Mange Kimambi aliye majuu,” aliimba.

Msanii huyo wa zamani wa WCB hata hivyo hatimaye alibainisha kuwa alikuwa akimtaniana tu malkia huyo wa bongo ambaye anadaiwa kuwa mpenzi wa Diamond.

Hii si mara ya kwanza kwa Rayvanny kumtania Zuchu wakati akitumbuiza jukwaani.

Wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania, Rayvanny alikiri kuwa alitaka kuanzisha vita  na aliyekuwa bosi wake Diamond ili amyakue  binti huyo wa Khadija Kopa.

"Mapenzi yanafanya nichanganyikiwe, niwe na uchu. Nilitamani nigombane na Simba, niende kwa Zuchu," aliimba Rayvanny.