Nilikuwa naandika wimbo wangu mpya 'Naringa' huku nikilia - Zuchu amefichua

"Hii kazi nilochagua moja ya changamoto yake ni kusemwa nikasema acha nihamishie hasira kwenye wimbo wangu .Nlikua naandika hii verse huku Nalia,” Zuchu alihadithia.

Muhtasari

• Msanii huyo alisema kwake kusemwa kumekuwa Baraka kwani asingepata wazo la kuandika wimbo huo pasi na kusemwa na watu.

Zuchu
Zuchu
Image: Insta

Malkia wa Bongo Fleva Zuchu amefichua kilichokuwa kinaendelea katika maisha yake wakati anaandika na kurekodi wimbo wake mpya wa Ninaringa.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu alipakia klipu ya sehemu ya wimbo huo na kufichua kwamba vesi hiyo alikuwa anaiandika akiwa na hasira za machungu ya kusemwa na walimwengu.

Msanii huyo alifichua kwamba kipindi cha siku chache zilizopita alikuwa akipambana na wakati mgumu wa kusimagwa mitandaoni na watu, jambo lililompa hasira kubwa na yeye kwa busara zake akaamua kuhamisha hasira hizo kwa wimbo wa Naringa – wimbo ambao amekiri kuuandika huku akilia.

Huu wimbo especially hii verse niliandika kipindi napitia wakati mgumu sana Kwenye hii kazi yangu ya mziki. Kama mnavowajua walimwengu hawakua mbali kunisema pia kipindi hiko bila ya kujali ubinaadamu. Ila sababu hii kazi nilochagua moja ya changamoto yake ni kusemwa nikasema acha nihamishie hasira kwenye wimbo wangu .Nlikua naandika hii verse huku Nalia,” Zuchu alihadithia.

Zuchu alitumia fursa hiyo kutema maneno ya busara kwa wafuasi wake akiwahimiza kutohuzunika pindi wanapogundua kwamba wanasemwa.

Msanii huyo alisema kwake kusemwa kumekuwa Baraka kwani asingepata wazo la kuandika wimbo huo pasi na kusemwa na watu.

“Yote ya Yote kusemwa pia ni Baraka mana inataka Nyota na kubarikiwa kusemwa na watu .Ukiona unasemwa au watu wanatumia nguvu kubwa kukuangusha jua Kuna kitu kikubwa umewashinda ndio maana wanakupiga vita . Anyways huu wimbo ukawape moyo na ujue kabisa wewe umechaguliwa na unaemtegemea Hapitiwi harogeki hapokei rushwa na hapendelei akisema Ndio Hakuna wa kupinga,” aliongeza.

Itakumbukwa wiki jana, Zuchu alikorofishana vikali mitandaoni na Mwijaku baada ya mtangazaji huyo mbwatukaji kumpa mamake Zuchu mzomo mitandaoni kisa kamruhusu bintiye kutembea kimapenzi na Diamond Platnumz kabla ya ndoa – jambo ambalo alisema limekatazwa na Allah.

Zuchu alisema kwamba alikuwa amemvumilia Mwijaku vya kutosha na kuahidi kutumia kila senti iliyoko kwenye akaunti yake kuhakikisha kwamba amemuadabisha Mwijaku kisheria kwa kile alisema ni kumuaibisha mamake.