Nadia Mukami afichua masomo ya Hisabati na Kemia yalikuwa yanamtii shuleni

“Nilikuwa msoma vitabu nilipokuwa shule ya upili. Mtaalamu sana wa Hisabati, Kemia, na Kiswahili lakini nilijitahidi katika masomo ya jamii." - Nadia alisema.

Muhtasari

• Alifichua kwamba alikuwa ni mwanafunzi aliyependa sana masomo kama Kemia, Kiswahili na Hisabati.

Nadia Mukami
Nadia Mukami
Image: Instagram

Nadia Mukami, mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za kizazi kipya na ambaye pia ni mjasiriamali wa lebo ya muziki ya Sevens Creative, Alhamisi alipata kuwarudisha mashabiki wake nyuma katika siku zake za awali akiwa kama mwanafunzi.

Alhamisi ni siku ambayo watu wengi hupiga kisengere nyuma katika maisha yao kuangalia na kutathmini hatua ambazo wamezipiga katika kupambania kuboresha maisha yao.

Kwa Mukami, ilikuwa ni safari ya kuwarudisha mashabiki enzi akiwa shule ambapo kwa kuwashangaza wengi, alidai kwamba alikuwa ni mwanafunzi aliyependa kubukua vitabu muda wote na hakuwahi kuwa na mpenzi wa kiume hadi pale alipokamilisha masomo.

Msanii huyo wa Radio Love alikiri kwamba babake ndiye alichangia pakubwa kutokuwa na mpenzi kwani alikuwa ni yule mzazi ambaye hapendi mchezo katika boma – muda wote kama haupo katika vitabu basi unajitafutia matatizo.

“Nilikuwa msoma vitabu nilipokuwa shule ya upili. Mtaalamu sana wa Hisabati, Kemia, na Kiswahili lakini nilijitahidi katika masomo ya jamii. Picha hii ilipigwa katika kituo cha KICD (kilichojulikana zamani kama KIE), ambapo baba yangu alikuwa akifanya kazi. Walikuwa na maktaba ambapo ningetumia likizo yangu. Nilikuwa ni mtu ambaye aliamini katika elimu juu ya pesa,” Mukami aliandika.

“Jinsi nilivyobadilika kuwa msanii, bado siwezi kufahamu. Nilikuwa mtu ambaye hata singeweza kuvaa suruali ya kubana, na sikuwa na mpenzi hadi nilipomaliza shule. Najua wote mnawajua watu wa aina hiyo.” Aliongeza kwa mshangao wa wengi.

Alifichua kwamba alikuwa ni mwanafunzi aliyependa sana masomo kama Kemia, iswahili na Hisabati.

Kilichovutia hisia za wengi ni kukiri kwake waziwazi kwamba alikuwa msichana mnyoofu ambaye hakuwahi kuwa na mpenzi wakati wa miaka yake ya shule ya upili na alikuwa akichukia nguo za kubana.

Ufichuzi wake ulichochea wimbi la hisia kutoka kwa mashabiki wake waliojitolea. Wengi waliachwa na mshangao wa mabadiliko yake ya ajabu kutoka mwanafunzi wa shule ya upili anayeonekana kuwa wa kitamaduni hadi kuwa msanii shupavu na anayejiamini ambaye yuko leo.