Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya amewajibu wale ambao wamekuwa wakikosoa kutojua kwake au tuseme kutotilia maanani kwake kuhusu ni nini mabadiliko ya hali ya hewa – mkutano ambao umekamilika Jumatano wiki hii jijini Nairobi.
Salasya alisema kwamba japo watu wanamuona mjinga katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, yeye katika nyanjani anachapa kazi kweli kweli kwa ajili ya wnanchi wake waliomchagua katika kura za mwaka jana Agosti.
Salasya alipakia picha na video mashine za kisasa zikiwachimbia kisima cha maji wananchi wake wa Mumias Mashariki na kusema kwamba yeye anachapa kazi bila kujali jinsi watu wanavyomuona.
“Wakati wa kampeni niliwaahidi wananchi wa Emutetemo kuwapa maji mara nitakapochaguliwa, kwa jamii ya Emutetemo na shule ya msingi ya Emutetemo wamepata shida ya maji tangu uhuru leo nimemwachia mkandarasi kufanya uchimbaji wa maji. Kama wengine wanavyofikiri ni mjinga linapokuja suala la #Climatechange lakini kazi ya msingi nachapa,” aliandika katika mtandao wake wa Facebook.
Salasya alikuwa amesema kuwa hivi majuzi alienda Mombasa na kulikuwa na baridi isivyo kawaida. Alipouliza, aliambiwa ni kutokana na Mabadiliko ya Tabianchi.
Haya ni maoni yale yale aliyoshiriki alipoulizwa kuhusu mkutano wa kilele wa hali ya hewa unaoendelea Nairobi.
"Nimeona watu wakinidhihaki kuwa sikujua chochote kuhusu mkutano huo. Ni kweli nilienda KICC kujivinjari, hali ya hewa sio eneo langu la wasiwasi. Sasa hivi niko hapa Kisumu kuangalia masuala ya sukari." , hiyo ndiyo inanihusu mimi, sio hali ya hewa," Salasya alisema kwenye video iliyoshirikiwa kwenye majukwaa yake ya mitandao ya kijamii.