Penzi la Marioo na Paula halitafika Desemba, Marioo ataishiwa hela - Baba Levo

Baba Levo anatoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya Paula kufichua kwamba tayari Marioo amezama mfukoni na kutoa hela shilingi milioni 100 kama mahari ya kumuoa.

Muhtasari

• Akitetea maoni yake, Baba Levo alisema kuwa vitatokea viwili kupelekea penzi lao kusambaratika kabla ya tamati ya mwaka.

Baba Levo atabiri kuachana kwa Marioo na Paula
Baba Levo atabiri kuachana kwa Marioo na Paula
Image: Maktaba

Chawa wa WCB Wasafi mwenye domo kama tarumbeta Baba Levo ameibuka na madai mapya kuhusu uhusiano wa msanii Marioo na binti wa muigizaji Fridah Masanja, Paula.

Akizungumza na waandishi wa habari za mitandaoni, Baba Levo alikiri tena bila kupepesa jicho kwamba penzi la wawili hao ambalo limekuwa likitajwa kama kiki halitofika mwezi Desemba mwaka huu.

Akitetea maoni yake, Baba Levo alisema kuwa vitatokea viwili kupelekea penzi lao kusambaratika kabla ya tamati ya mwaka.

“Penzi la Marioo na Paula halitofika mwezi wa kumi na mbili. Ni vitu viwili, ama Marioo atakuwa ameishiwa hela kabisa na kuwa ombaomba, au ndugu yetu [Paula] atapata mtu mwingine mwenye hela Zaidi,” alisema akiashiria kwamba huenda Marioo anachunwa kushoto kulia na kibubu chake cha hela kimekuwa chepesi.

Baba Levo ambaye ni mtetezi mkali wa sera za WCB Wasafi alisema kuwa ana ushahidi wa jinsi Paula na mama yake walivyo na historia ya unyonyaji wa mali za mwanamume anayekanyaga kwenye anga zao akisema aliliona hilo hata katika Rayvanny kipindi Paula wanachumbiana naye.

“Niliona Rayvanny kuna muda alikuwa anaendesha gari akiongea peke yake. Kwa namna ambavyo alikuwa ameshapigwa mizinga, unapigwa mzinga huku chini unapigwa juu unapigwa kushoto unapigwa kwa mama, mtoto anakushambulia,” Baba Levo alisema.

Alisema eti Rayvanny kwa kipindi kimoja ilibidi amfuate na kumuomba ushauri akisema kuwa nusra alikuwa afe kutokana na msongamano wa mahitaji ambayo alikuwa anatakiwa kutekeleza kwa Paula na mama yake.

“Aliniambia huku naona nitakufa Baba Levo, huku naombwa sijui chuo, huku sijui hela ya habaya… alibaki hpi, alichanganyikiwa,” alisema.

Baba Levo anatoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya Paula kufichua kwamba tayari Marioo amezama mfukoni na kutoa hela shilingi milioni 100 kama mahari ya kumuoa.

Marioo hata hivyo hajathibitisha hilo lakini kwa mara kadhaa tu amekuwa akisema kuwa Paula anampunga kwa mahaba yenye hadhi ya nyota tano na huenda akamuoa mapema kuliko muda aliokuwa amejiratibia kuoa.