Eric Omondi akamatwa na polisi akipatiana petroli ya bure kwa wana bodaboda Lang'ata

Omondi alisema kwamba alikuwa anawanunulia mafuta vijana wa bodaboda kila mmoja mafuta ya shilingi 300 ili kuwasukuma kidogo wakati ongezeko la bidhaa hiyo limewafukuza wengi barabarani.

Muhtasari

• Omondi alikuwa akiwanunulia petroli waendesha bodaboda hao ambao walikuwa wamepanga foleni.

• Ghafla maafisa wawili wa polisi walimvizia na kumtia nguvuni huku wanabodaboda hao wakijaribu kumtetea asikamatwe.

Eric Omondi akamatwa
Eric Omondi akamatwa
Image: Insta

Kwa mara nyingine tena mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi amejipata katika mkono mbaya wa dola baada ya afisa wa polisi waliokuwa wanapiga doria eneo la Lang’ata kumtia mbaroni alipokuwa akiwanunulia mafuta ya petroli wahudumu wa bodaboda.

Katika video ambazo zimeenezwa kwenye mitandao ya kijamii, Omondi alikuwa katika kituo cha mafuta cha Ola akiwa amezingirwa na makumi ya waendesha bodaboda.

Omondi alikuwa akiwanunulia petroli waendesha bodaboda hao ambao walikuwa wamepanga foleni.

Ghafla maafisa wawili wa polisi walimvizia na kumtia nguvuni huku wanabodaboda hao wakijaribu kumtetea asikamatwe.

Akizungumza na mwandishi wa habari za mitandaoni, Vincent Mboya, Omondi alisema kwamba alikuwa anaelekea nyumbani wakati alipatana na mhudumu mmoja aliyekuwa akilia kuhusu pikipiki yake kutokuwa na mafuta.

Aliamua kuongozana naye hadi kituo hicho cha mafuta lakini ghafla akapata wengine wengi wamemzingira wakimlilia kwa tatizo lilo hilo.

“Niko Lang’ata hapa nawekea watu mafuta, kila mtu 300 itamsukuma kidogo juu sasa maisha yamekuwa magumu. Nilikuwa naenda nyumbani na kijana mmoja anasukuma pikipiki nikamuuliza imeharibika akasema ni mafuta imemaliza, ndio nikapata wazo la kuja kufanya hivi,” Omondi alimwambia Mboya.

Ikumbukwe Wakenya wengi mwishoni mwa wiki jana walipigwa na butwaa baada ya mafuta kupanda bei mara dufu na kufikisha bei ya kihistoria ya Zaidi ya shilingi 200 kwa lita kwa mara ya kwanza nchini Kenya.

Ongezeko hilo la bei mara dufu limewafanya wengi kuhisi mzigo mzito wa gharama ya maisha ambapo sasa bei za bidhaa na huduma mbali mbali zikiwemo zile za uchukuzi wa umma zikiongezeka na kuwaacha Wakenya hoi.

Kwa upande wake, Omondi licha ya kukanusha kumezea mate kiti cha ubunge Lang’ata amekuwa akionekana akifanya shughuli za hisani kwa baadhi ya watu.

Kando na hili la kuwanunulia petroli wahudumu wa bodaboda, Omondi pia aliwahi onekana akiwataka watu kufunga barabara ili kutoa nafasi kwake kuwagawia unga, wakati bei ya bidhaa hiyo ilikuwa inakaribia shilingi 250 kwa pakiti ya kilo mbili.

Wengi wamekuwa wakihisi hii ni njia moja ya kuuza sera zake kwa watu wa Lang’ata kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 ambapo analenga kumng’atua mamlakani mbunge wa sasa Phelix Odiwuor maarufu Jalang’oo.