Tasnia ya muziki nchini imetupwa katika kipindi cha majonzi na maombolezo kufuatia kifo cha produsa wa miziki ya kizazi kipya kwa jina Byron.
Byron ndio fundi nyuma ya vibao hodari kama vile Sipangwingwi chake Exray – kibao ambacho kilimvutia Rais Ruto hadi kukitumia katika kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Amefanya kazi na wasanii wakuu wa Kenya kama vile Mejja, Ssaru, X-ray, Trio Mio na wengine.
Taarifa za kifo chake zilivujishwa mitandaoni ambapo mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya nchini maarufu kama Gengetone walimuomboleza kama jamaa aliyekuwa na ubunifu wa aina yake katika kuzalisha midundo ya kipekee.
Msanii mkongwe wa muziki Juacali alimuomboleza Byron kama produsa muelewa akifichua kwamba katika albamu yake ya hivi majuzi ya ‘Utu Uzima’ Byron alizalisha midundo kwa ngoma zake mbili.
“Siku ya kusikitisha leo kwa Sekta ya Muziki ambayo ndiyo kwanza inapata Habari ByronOnTheBeat amefariki dunia. Ametoa nyimbo 2 kwenye albamu yangu ya UTU UZIMA ‘TARANTELA na MALKIA’ May his soul RIP,” JuaCali aliandika kwenye mitandao yake ya kijamii.
Mbali na utengenezaji wa muziki, Byron pia alikuwa mwimbaji-mtunzi wa nyimbo mwenye talanta.
Mtindo wake wa muziki ulikuwa Dancehall, Afro-Pop na Afro-Fusion. Dhamira yake ilikuwa kutengeneza nafasi kwa Muziki wa Kenya katika soko la kimataifa.
Sababu ya kifo bado haijawekwa wazi. Wakenya kwenye mitandao ya kijamii na wasanii wa Kenya wakiwemo genge la Boondocks wameshiriki jumbe zao za rambirambi.