Kate Actress athibitisha yeye na Director Phil Karanja si wapenzi tena!

Kate Actress ameolewa na Phillip Karanja, mkurugenzi wa filamu na mwigizaji wa zamani wa Tahidi High tangu Novemba 17, 2017. Hafla yao ya fungate iliadhimishwa nchini Ushelisheli.

Muhtasari

• Kate alipakia ujumbe huo uliokuwa na maandishi kwamba ni kutoka kwa pande zote, yeye na Phil na kuwataka mashabiki wao kukubaliana na uamuzi wao.

Kate Actress na Director Phil
Kate Actress na Director Phil
Image: Insta

Mwigizaji na mjasiriamali Catherine Kamau maarufu kama Kate Actress amethibitisha kwamba ni kweli yeye na mpenzi wake ambaye ni muongozaji wa video, Phil Karanja si wapenzi tena.

Kate aliweka haya wazi kupitia insta story zake ambapo alipakia ujumbe wa kuthibitisha hilo akisema kwamba ni kweli waliachana muda mrefu sasa umepita ila waliafikiana kuliweka suala hilo kinyemela ili kushughulikia masuala Fulani.

Kate alipakia ujumbe huo uliokuwa na maandishi kwamba ni kutoka kwa pande zote, yeye na Phil na kuwataka mashabiki wao kukubaliana na uamuzi wao kwamba mambo yalishindwa kutengemaa.

“Tulifikia uamuzi wa kuvunja ndoa yetu muda mrefu uliopita na tukatengana. Kwa kweli tunaomba kila mtu kuheshima uamuzi wetu kwa ajili ya maisha yetu ya faraghani lakini pia na ya watoto wetu,” ujumbe huo mfupi ulisoma.

Itakumbukwa wiki kadhaa baada ya kuteuliwa kama mwanachama katika  baraza la Talanta Hela na waziri Ababu Namwamba, baadhi ya mashabiki waliibua uvumi kwamba Kate Actress alionekana kujitenga na mpenziwe Phil Karanja, uvumi ambao hata hivyo ulififia hata kabla ya kuchanua.

Sasa Kate amethibitisha kwamba uvumi huo wa kuachana kwao muda ulikuwa ni kweli lakini akasisitiza kwamba waliweka siri ili tu kunyoosha baadhi ya vipengele katika kazi zao na sasa ni muda mwafaka wa kuweka wazi kwamba hawapo pamoja tena.

“Haikuwa siri, ni kweli tuliachana muda mrefu. Tuliamua kuliweka faraghani. Kwa mashabiki wetu wote, ahsanteni sana kwa kutuunga mkono katika miaka hii yote,” Kate alisema.

Catherine Kamau maarufu kama Kate Actress ameolewa na Phillip Karanja (maarufu Phil au Melvin), mkurugenzi wa filamu na mwigizaji wa zamani wa Tahidi High tangu Novemba 17, 2017.

Hafla yao ya fungate iliadhimishwa nchini Ushelisheli.