Diamond Platnumz hana hisa hata kidogo katika kampuni yetu - Ziiki Media wacharuka

“Diamond alipoanza taaluma yake alianza na Ziiki, kwa hiyo Ziiki ndio ilikuwa inamsaidia kusambaza miziki yake, kwa hiyo tumekuwa na uhusiano na Diamond tangu alipoanza."

Muhtasari

• Kando na Diamond, pia walikanusha madai ya Harmonize kwamba Ziiki na WCB Wasafi waliiba pesa zake za kusambaza miziki yake.

• “Kumbuka akiwa WCB, Ziiki ilikuwa inafanya kumsambazia kazi zake na pia mpaka sasa hivi tunafanya kusambaza kazi yake,” alisema.

Ziiki
Ziiki
Image: Screengrab

Kampuni ya jukwaa la kusambaza muziki wa wasanii kwa njia za kijiditali ya Ziiki Media wamekanusha madai ambayo yamekuwa yakiendeshwa kwa muda mrefu kwamba msanii namba moja wa Bongo Fleva Diamond Platnumz ana hisa katika kampuni hiyo.

Wakizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari nchini Tanzania alasiri ya Jumatano, Ziiki walinyoosha maelezo wakisema kwamba uvumi huo ni wa kupotosha kwani Diamond kama tu wasanii wengine yuko kwenye Ziiki kimkataba kwa ajili ya kusaidiwa katika usambazwaji wa kazi zake za muziki.

“Diamond Platnumz hana hisa zozote katika kampuni yetu ya Ziiki media. Naomba mnisikilize kwa makini na hilo lieleweke. Naomba baada ya leo hiyo isiwe kwenye mazungumzo. Kwenye kampuni yetu kuna muasisi anaitwa Arun Nagar. Yeye ndiye muasisi na CEO wa kampuni yetu. Na investiment imefanywa na Werner Music Global na hao ndio tu wako na hisa kwenye Ziiki lakini Diamond ni msanii mwenye ako chini ya Ziiki,” walisema.

Walikwenda mbele kuhadithia safari ndefu ambayo Ziiki na Diamond wametembea, wakifichua kwamba msanii huyo akianza taaluma yake takribani miaka 15 iliyopita, Ziiki ndio walikuwa wanamsambazia miziki yake kwenye masoko ya kidijitali.

“Diamond alipoanza taaluma yake alianza na Ziiki, kwa hiyo Ziiki ndio ilikuwa inamsaidia kusambaza miziki yake, kwa hiyo tumekuwa na uhusiano na Diamond tangu alipoanza ndio maana pengine watu wanasema Diamond ana hisa Ziiki, hana hisa hata kidogo,” msemaji wao alisema.

Kando na Diamond, pia walikanusha madai ya Harmonize kwamba Ziiki na WCB Wasafi waliiba pesa zake za kusambaza miziki yake.

Itakumbukwa Harmonize alitangaza vita na Ziiki akisema kuwa tangu aondoke Wasafi, wimbo wake mkubwa Zaidi wa Kwangwaru hajawahi pata mapato kwani yalikuwa yanaingia katika mifuko ya watu Fulani licha ya kwamba alikatisha mkataba WCB, alilipia kila kitu zikiwemo hatimiliki za wimbo.

“Kumbuka akiwa WCB, Ziiki ilikuwa inafanya kumsambazia kazi zake na pia mpaka sasa hivi tunafanya kusambaza kazi yake,” alisema.