Unapendwa ukishakufa!: Ngoma 3 za Mohbad zaingia kwenye 10 bora chati ya Billboard

Hii ndio ilikuwa mara ya kwanza kwa nyimbo za msanii huyo kuingia kwenye Billboad, ikiwa ni umaarufu kutokana na kifo chake chenye utata.

Muhtasari

• Baada ya kufa kwake kwa njia tatanishi, kifo chake kimevutia wengi wasiokuwa wanamjua kuchimbua Zaidi ili kumjua.

• Wimbo mwingine wa Mohbad unaopendwa sana, Feel Good, pia ulionekana kwa mara ya kwanza kwenye chati ya muziki ya Billboard.

Moh Bad
Moh Bad
Image: Instagram

Wenye midomo walishasema, katika ulimwengu wa sasa, mtu anaoneshwa upendo mkubwa baada ya kufa. Unaweza ukafa leo hii kwa ajili ya njaa lakini kesho kwenye msiba wako, wakapika wali, pilau na nyama wakala na kushiba.

Ndio hali ambayo inashuhudiwa kwa mchezaji chipukizi Mohbad kutoka Nigeria ambaye alikuwa anahangaika kutusua kimuziki chini ya lebo ya mchezaji mwenza Naira Marley.

Baada ya kufa kwake kwa njia tatanishi, kifo chake kimevutia wengi wasiokuwa wanamjua kuchimbua Zaidi ili kumjua.

Hili limepelekea nyimbo zake ambazo kabla ya kifo hazikuwa kubwa hihivyo lakini sasa kutokana na kusikilizwa na watu wengi wanaotaka kujua Mohbad ni nani, ngoma hizo zimekwea katika chati za Billboard.

Wiki moja tu baada ya nyota huyo wa muziki mwenye talanta kufariki, nyimbo zake zilifika kwenye chati ya muziki ya Billboard kwa mara ya kwanza.

Hivi majuzi Billboard walishiriki chati yao ya nyimbo zinazovuma zaidi inayoendeshwa na Twitter, ambayo sasa inajulikana kama X, na Mohbad alishinda nafasi tatu kati ya nyimbo 10 bora zilizoorodheshwa.

Peace ya Mohbad, iliyotolewa mwaka wa 2022 chini ya lebo ya Marlian Music, imepata umaarufu baada ya kifo cha mwimbaji huyo. Wimbo huo umeshika nafasi ya 3 kati ya nyimbo 10 bora kwenye chati ya Billboard.

Baadhi ya mashabiki wamechambua mashairi yake ili kubaini ikiwa aliimba kuhusu magumu aliyokuwa akikumbana nayo maishani kabla ya kuangamia kwake.

Wimbo mwingine wa Mohbad unaopendwa sana, Feel Good, pia ulionekana kwa mara ya kwanza kwenye chati ya muziki ya Billboard.

Feel Good ilitolewa mnamo 2021, pia chini ya Marlian Music. Nyimbo za Mohbad zinazungumza kuhusu yeye kuwa na maadui wengi anaowakimbia. Wimbo huo pia umejinafasi katika nambari 5 kati ya nyimbo 10 za Billboard wiki hii.

Pia aliimba kuhusu kuwa mtu maarufu na anayetafutwa licha ya kuwa hajulikani hapo awali. Feel Good bila shaka ni kipenzi cha mashabiki.

Pia kwenye chati ya nyimbo zinazovuma katika Billboard kuna wimbo wa Mohbad, Ask About Me. Wimbo huu ulitolewa mnamo 2023 na Mohbad kama msanii huru baada ya kuachana na Marlian Music kwa masharti ya kutatanisha.

 Ask About Me pia imekuwa video ya nne bora ya muziki kwenye YouTube wiki moja tu baada ya kifo cha mwanamuziki huyo kwa bahati mbaya. Kwenye Billboad, wimbo huo uko katika nafasi ya 8.