Harmonize aombewa msamaha kwa Diamond

"Tumeshamsamehe hata huyo Konde Boy mwenyewe. Diamond msamehe bosi wangu, msamehe ni kijana wako, umemtotoa msamehe, ahsante,” Baba Levo alimwambia.

Muhtasari

• “Bila Diamond njaa ingeniuwa. Baba Yetu wa mbinguni tusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea." aliimba.

Harmonzie, Diamond Platnumz
Harmonzie, Diamond Platnumz
Image: Instagram

Chawa wa WCB Wasafi na msanii Diamond Platnumz, Baba Levo baada ya kutoa wimbo wa Amen na Diamond, amechukua fursa hiyo kumsihi bosi huyo wake kumsamehe Harmonize baada ya kuvurugana mwishoni mwa mwaka 2019.

Baba Levo alikuwa akitumbuiza wimbo huo jukwaani kwa mara ya kwanza katika tamasha la Wasafi Festival na alimshukuru Diamond kwa kumshika mkono akisema kwamba bila yeye njaa ingemuuwa.

Alikiri kwamba wimbo huo si wa mbwembwe bali unakaa kiinjili Zaidi na kumtaka Diamond kumsamehe hata na Harmonize kama ambavyo Mungu anawasamehe watu wake.

“Bila Diamond njaa ingeniuwa. Baba Yetu wa mbinguni tusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe waliotukosea. Tumeshamsamehe hata huyo Konde Boy mwenyewe. Diamond msamehe bosi wangu, msamehe ni kijana wako, umemtotoa msamehe, ahsante,” Baba Levo alimwambia Diamond jukwaani moja kwa moja huku Diamond akibaki na tabasamu pana usoni.

Itakumbukwa Diamond na Harmonize walikuwa washikaji wakubwa sana mapema miaka ya 2010s lakini walikuja kuvurugana kuhusiana na miamala mwaka 2019 kupelekea kuchipuka kwa uadui wao wa kimuziki.

Baada ya kuondoka Wasafi, Harmonize alishiriki mirundiko ya mahojiano na vyombo vya habari akisema kwamba alikuwa anapunjwa maokoto yake pale Wasafi na hata baada ya kuvunja mkataba, alilazimika kulipa shilingi milioni 600 za Tanzania ili kupewa hakimiliki za kazi zake pamoja na mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, Diamond hajawahi kuzungumzia bayana ugomvi wao lakini kila mahali anakokwenda, anajibunia sana mafanikio ya Harmonize akijiita kama baba anayefurahi mafanikio ya mtoto aliyemkuza.

Diamond alisema kwamba yeye hana uadui wowote na Harmonize bali ni mitikasi tu ya kila mmoja kujipambania na kutafuta riziki, akisema kwamba kwa kiasi Fulani katika tasnia ya Bongo ili muziki wako uende, lazima utafute kulazimisha bifu na mtu.