Esther Musila amchekelea mtu aliyemwambia ni mzee na ameharibu maisha ya Guardian

Musila mwenye umri wa miaka 53 alifunga harusi ya faraghani na msanii Guardina Angel mwenye umri wa miaka 33 mapema mwaka 2022 na wamekuwa wakipokea maneno ya shombo kutoka kila kona.

Muhtasari

• “Hehehehehe hebu njoo mnisaidie kumcheka huyu,” Musila alisema huku akiendeleza kicheko kirefu cha kebehi na dharau.

• Licha ya kutupiwa maneno ya kila aina, wawili hao wameonekana kuzidisha mapenzi yao kila kuchao.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel.
Esther Musila na mumewe Guardian Angel.
Image: Insta

Esther Musila amekuwa akionesha kutobabaishwa kwake na wakosoaji wa mitandaoni ambao mara kwa mara hutupa makombo kwenye uhusiano wake na mume wake Guardian Angel.

Licha ya kutupiwa maneno ya kuchukiza na wakosoaji haswa kuhusu tofauti kubwa ya umri wake na msanii huyo wa injili, Esther amekumbatia kutoweka rohoni ukosoaji huo na sasa amekuwa jasiri kiasi kwamba ameanza kuwajibu shombo vilevile wale wanaomletea za hovyo.

Hivi majuzi, Musila alikuwa anafanay vipindi vyake kwenye TikTok wakati mtumizi mmoja wa mtandao huo alipomwandikia ujumbe wa kumghasi kwamba yeye amechangia kwa kiasi cha haja kuharibu na kuvuruga maisha ya muziki na ya kibinafsi ya msanii Guardian Angel.

Mkosoaji huyo pia alikwenda mbele kumuingia kwenye maini Zaidi Musila kwa kumwambia kwamba yeye na Guardian Angel hawaendani hata kidogo, akipiga pale pale kwenye mshono kwamba yeye ni mzee na anafaa kumuachia kijana wa watu ili kutafuta rika lake wa kuoana naye.

“Umeharibu kabisa maisha ya Guardian Angel, pia wewe ni mzee sana kwake,” shabiki huyo alimwambia.

Wengi wangedhani kwamba Musila angeonesha chuki na kuchemka kwa maneno makali kwa shabiki huyo lakini alichokifanya ni kumchekea kwa dharau na kuwataka mashabiki wake kujiunga naye ili kumcheka huyo ambaye anamwambia kitu ambacho amekuwa akikisikia kwa muda na ambacho sasa hakionekana kuwa na athari yoyote kwa uhusiano wake na Guardian.

“Hehehehehe hebu njoo mnisaidie kumcheka huyu,” Musila alisema huku akiendeleza kicheko kirefu cha kebehi na dharau.

Musila mwenye umri wa miaka 53 alifunga harusi ya faraghani na msanii Guardina Angel mwenye umri wa miaka 33 mapema mwaka 2022 na wamekuwa wakipokea maneno ya shombo kutoka kila kona lakini penzi lao linaonekana kukolea munyu kila sekunde iendayo kwa Mungu.