Msanii wa injili ya Kikuyu, Kigooco, Betty Bayo amewazuzua mashabiki katika mtandao wa TikTok baada ya kupakia video akimjibu kwa shombo shabiki ambaye alimkejeli kwa kuolewa akiwa na watoto wawili kutoka ndoa ya awali.
Bayo ambaye alioleka mwishoni mwa mwaka 2021, ikiwa ni miaka 6 baada ya kuvunja uhusiano wake na mchungaji mwenye utata Victor Kanyari – ambaye ndiye baba wa wanawe wawili alimjibu shabiki huyo kwamba siku hizi watu huoleka hata wakiwa na watoto 10 na ndio ukweli usiofichika.
Shabiki huyo alikuwa anatumia nadharia ya mchezo wa soka akisema kwamba timu zote zinapoingia uwanjani kabla ya kipenga kupulizwa, kila timu huwa na bao sufuri bin sufuri, lakini kwa Bayo, mechi yake ilianza tayari akiwa na mabao [watoto] mawili.
“Hakuna mechi huanza 2-0,” shabiki huyo alimwambia kwa kejeli.
“Situmwambia huyu ukweli, siku hizi hata 10-0 mechi huanza bado,” Bayo alijibu huku akiweka wimbo wa Ringtone na Rose Muhando “sisi ndio tuko,” kama njia moja ya kuongeza nguvu na uzito kwenye jibu lake kwamba wanawake wenye watoto siku hizi ndio wanaolewa tena bila taswishi.
Msanii huyo alizidi kumueleza jamaa huyo aliyemkejeli kuoleka na watoto kwamba Biblia inasema hakuna mtu ambaye hatakosa mpenzi duniani.
Mashabiki wake walifurika kwenye upande wa kutoa maoni wakifichua jinsi ndoa zao ziliacha zikiwa tayari na mabao [watoto] na zingine zikiwa hadi sasa zimesimama tisti.
“Kina mama kwa watoto wawili ndio tunatesa siku hizi,” Olive Valentine.
“Yangu ilianza na 2-2 na ni miaka 10 sasa na tunaendelea,” Shiku Muthoni.
“Ya mamangu ilianza 4-0 tangu mwaka 2004 na naweza nikabashiri kwamba nimekuwa na baba mzuri zaidi. Nampenda sana sasa hivi kwamba tushakua watu wazima,” Veronica.
Bayo waliachana kwa njia ya kishari na mchungaji Victor Kanyari kufuatia Makala ya ufichuzi ambayo yalifanywa na Jicho Pevu kuhusu ukora na ulaghai wa kiroho ambao ulikuwa unafanywa katika kanisa la mchungaji huyo.