Aslay ajibu kubembelezwa na Diamond kuingia Wasafi, "Ni heshima kubwa sana!"

“Kwanza ile kauli nilivyoisikia [kwamba Diamond aliwahi nifuata kunitaka WCB] niliona kama ni heshima kwangu" Aslay alisema.

Muhtasari

• “Endapo itatokea kama lolote linaloweza kutokea kwa sababu ya kazi tu, niko tayari kufanya kazi na mtu yeyote,” alisema.

Aslay na Diamond
Aslay na Diamond
Image: Screengrab

Kwa mara ya kwanza Aslay amenyoosha maelezo kuhusu uvumi ambao umekuwa ukiendeshwa kwa muda mrefu kuhusu yeye kutimukia lebo ya Diamond Platnumz, WCB Wasafi.

Msanii huyo ambaye yuko kwenye media tour kuipigia debe shoo yake ya mwisho wa mwezi huu ya kuadhimisha miaka 10 kwenye tasnia ya Bongo Fleva alifunguka haya katika kipindi cha Amplifaya cha Clouds.

Mwanzo alitenganisha maji na unga kuhusu dai la kufuatwa na Diamond ili kusaini kama mmoja wa wasanii wa WCB Wasafi lakini pia akasema kwamba Diamond kutambua uwezo wake kimuziki ni heshima kubwa sana.

“Kwanza ile kauli nilivyoisikia [kwamba Diamond aliwahi nifuata kunitaka WCB] niliona kama ni heshima kwangu. Yaani mpaka anajua kama mimi nina kipaji kikubwa halafu yeye ni mtu ambaye keshapita sehemu nyingi na keshatembea nchi nyingi na kuona vingi, kujua kama kuna mtu ana kipaji namna hii kwangu ni heshima, kwa hiyo kauli hiyo sijaifikiria kwa ubaya na sijaona baya lolote aliloliongea,” alisema.

“Diamond ni mtu mkubwa, ana uwezo wa kufanya kitu chochote na kwa wakati wowote na kikawa kikubwa. Kwa hiyo kutamani kunisaini WCB kwa sasa hivi hapana. Tayari nina malengo yangu na nina vitu vyangu ninavyotarajia kuvifanya. Lakini sijawahi fuatwa na Diamond kwamba anataka kunisaini wala watu wake hawajawahi nifuata,” aliongeza.

Lakini pia Aslay alikiri kwamba endapo kitatokea kitu chochote kwenye mzunguko wa maisha ya Sanaa basi yuko tayari kufanya kazi na msanii yeyote hata Diamond mwenyewe.

“Endapo itatokea kama lolote linaloweza kutokea kwa sababu ya kazi tu, niko tayari kufanya kazi na mtu yeyote,” alisema.