Huwa inaniuma sana Wakisii wenzangu wakiniona na kusema 'ficha huyo' - Embarambamba

"Walinichomea wakasema huyo ni wazimu msimpeleke kwa rais wakati alikuwa na sherehe kubwa huko Kisii. Walichoma hadi nikatolewa kwenye ratiba ile ya watumbuizaji wa rais,” alisema kwa uchungu.

Muhtasari

• "Mimi Kisii sijafanya hii mikutano nafanya ya crusade na sijaenda mkutano wowote kwa sababu zamani nilichomewa" alisema.

Embarambamba.
Embarambamba.
Image: Screengrab

Msanii mwenye sarakasi katika muziki wa injili kutoka kaunti ya Kisii Embarambamba amefichua kwamba japo anapendwa na mashabiki wake kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi, nyumbani kwao huwa hawampendi hata kidogo.

Msanii huyo alisema kwamba amefanya shoo na kutumbuiza katika sehemu nyingine ambako anaalikwa lakini hakuna shoo ya mahubiri hata moja ambayo amewahi kualikwa nyumbani kwao Kisii.

Alifichua haya katika mahojiano na chaneli ya 2Mbili na kukiri kwamba kitu hicho humuuma sana watu wa kabila lake wanapomlinganisha na mwendawazimu na kusema afichwe pindi wanapomuona.

Alikumbuka jinsi watu wa kabila lake walimchomea picha wakati Ruto alikuwa anazuru Kisii wakisema kwamba yeye ni wazimu na hangefaa kupewa mwaliko wa kutumbuiza Katika mkutano wake.

“Ni ukweli Wakisii wenzangu wakiniona wanasema ‘ficha huyu’ na ni huwa nasikia uchungu sana. Mimi Kisii sijafanya hii mikutano nafanya ya crusade na sijaenda mkutano wowote kwa sababu zamani nilichomewa. Walinichomea wakasema huyo ni wazimu msimpeleke kwa rais wakati alikuwa na sherehe kubwa huko Kisii. Walichoma hadi nikatolewa kwenye ratiba ile ya watumbuizaji wa rais,” alisema kwa uchungu.

“Tangu siku hiyo mimi sijawahi kualikwa sherehe nyingine Kisii kwetu, labda nisikie sherehe iko mahali nijipeleke, lakini kualikwa sijaona Mkisii akinialika,” aliongeza.

Msanii huyo alisema kwamba amealikwa karibia maeneo yote humu nchini kando na nyumbani na kudai kwamba sasa hivi ndio watu wao wameanza kuonesha kujuta kwa kutomualika siku za nyuma kwa kuona kwamba anapendwa mbali na nyumbani.

“Hawa makabila wote wamenialika, Wakisii sasa hivi ndio wanaona kwamba ni kama anapendwa nje kuliko sisi tuliomzaa. Sasa wameanza kufikiria,” alisema.