Msanii na mtunzi wa nyimbo Nadia Mukami amefunguka kuhusu uhusiano wake na wasanii tajika wa kike wa Tanzania Zuchu na Nandy.
Nadia ambaye amerejea nchini baada ya kuibuka mshindi wa tuzo ya Afrika kitengo cha wanawake Afrika Mashariki amaesema awezi akashusha heshima aliyonayo kwa wasanii maarufu aliowashinda kwenye mashindano hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa ndege wa Kimataifa JKIA,Nadia amesema kuwa msanii Zuchu na Nandy ni dada zake kimziki na hivyo anawatambua.
Ameeleza kuwa hawezi akashusha heshima yake kwa sababu wanafanya kazi pamoja, akisema kwamba kuna ngoma ambayo wanaandaa yeye pamoja na Nandy.
"Ni dada zangu,hasa Nandy kuna ngoma tunaandaa na yeye,kwa hiyo siwezi nikawadhalilisha dada zangu. Sio sifa zangu kudhalilisha wanawake walio kwenye tasnia ya muziki,muda mwingine ni matani ya mitandaoni tu ila nawaheshimu." Alisema
Hivi majuzi,Nadia alidai kuwa yeye ni msanii tajiri Afrika Mashariki na kusema kwamba hakuna msanii wa kike Afrika Mashariki anamshinda kifedha.
Kutokana na kauli hii pamoja na ushindi wake uliowabwaga mabingwa tajika kwenye tasnia hiyo ya muziki Afrika Mashariki, mashabiki walidhania kuwa Nadia angetema moto kwa wenzake,jambo ambalo alikanusha kwenye mazungumzo.
Nadia Mukami alirejea nchini baada ya ziara yake wiki mbili Marekani alikoenda kwa ajili ya sherehe ya tuzo za AFRIMMA.
Alisema kuwa si jambo la busara wasanii kudhalilishana ila ni muhimu wao kushirikiana kuhakikisha tasnia ya muziki Afrika inatamba.