Ni kawaida, Khadija Kopa asema baada ya Zuchu kurushiwa jiwe steji

Khadija Kopa aliwashauri wasanii kuvumilia maovu yote watakayokumbana nayo kutoka kwa mashabiki wao .

Muhtasari

• Zuchu alirushiwa jiwe  wakati alipokuwa akitumbuiza kwenye jukwaa mjini Mbeya katika tamasha la Wasafi Festival 2023.

 

Khadija Kopa na binti yake Zuchu

Khadija Omari  Kopa   mwimbaji wa muziki wa Taarab na mtunzi wa nyimbo kutoka nchini Tanzania ambaye pia ni  mamake mzazi msanii maarufu wa Bongo Zuchu amezungumzia kisa cha mwanawe kurushiwa jiwe akitumbuiza wafuasi wake.

Zuchu alirushiwa jiwe  wakati alipokuwa akitumbuiza kwenye jukwaa mjini Mbeya katika tamasha la Wasafi Festival 2023 jambo lililomkera na kumlazimu kushuka kwenye jukwaa.

Kulingana na maoni ya  Khadija Kopa ambaye ni mwimbaji wa muda mrefu jambo hilo ni la kawaida kwa wasanii wakubwa wanaotumbuiza kwa jukwaa lenye wafuasi wengi.

"Jambo la kurushiwa maji,mawe au pia kuvutwa nywele ni kawaida kwa wasanii, wengi wa wale wafuasi hufanya lile jambo ili waonekane lakini wengine pia hupagawa na furaha baada ya kunywa pombe jambo ambalo linawafanya kutenda vitendo kama hivyo kwa hivyo wasanii watarajie makubwa". alisema Khadija kopa.

Kwenye mahojiano ya moja kwa moja Khadija Kopa aliwashauri wasanii kuvumilia maovu yote watakayokumbana nayo kutoka kwa mashabiki wao .

Mashabiki wengi waliofika kwenye tamasha hilo walisitikishwa na jambo hilo liliofanywa na mmoja wa shabiki baada ya msanii Zuchu kutoka jukwaani alipokuwa akisakata ngoma huku akiwatumbuiza kwa wimbo wake Honey.