Mwanablogu na mwandishi wa habari za mitandaoni, Nicholas Kioko ametangaza kuwa mwishoni mwa mwaka huu, yeye na mama wanawe mapacha Wambo Ashley watafanya uhusiano wao wa kimapenzi kuwa rasmi kwa kufanya bonge la harusi.
Wawili hao katika ujumbe wa pamoja ambao walishiriki katika mtandao wa Instagram, walitangaza kwamba Desemba 29, siku mbili tu kabla ya kukunja jamvi la mwaka wa 2023, itakuwa ni siku yao kubwa.
Walipakia kadi ya mwaliko, wakisema kwamba itakuwa siku ya kurasmisha kila kitu na kuanza safari ya kuwalea wanao mapacha wa kiume.
“Pamoja na familia zao, bwana na bi Nicholas Kioko na Wambo Ashley wanaomba uwepo wenu kwa sherehe ya harusi yao itakayofanyika Jumamosi Desemba 29 majira ya saa nne asubuhi,” sehemu ya kadi hiyo ya mwaliko wa harusi ilisoma.
Wapenzi hao ambao wamekuwa pamoja kwa muda walitangaza mwaka jana taarifa njema za kubarikiwa na mimba ya mapacha.
Baadae walikuja kufichua kwamba mapacha wao ni wa kiume na hivi majuzi pia walishiriki kwa mara ya kwanza picha za watoto hao ambao kwa kiasi kikubwa wanamfanana baba yao, Nicholas Kioko.
“Mapacha ni baraka kutoka kwa Mungu. Wao pia ni wa ajabu sana. Kutana na mapacha wetu hatimaye @rom_twins,” wakiandika wakati wa kutambulisha nyuso za mapacha hao kwa mashabiki wao wa mitandaoni kwa mara ya kwanza.