Vanessa Mdee asimulia safari ndefu na ngumu ya kuwalea wanawe wawili

"Kukosa kupumzisha akili yako kwa sababu iko kazini usiku na mchana. Kuwa mama ni kazi 100 ndani ya moja,” aliongeza.

Muhtasari

• Mdee alitumia fursa hiyo kutoa ujumbe wa himizo kwa kina mama wengine ambao wanahisi kuchoka kwa malezi.

Vanessa Mdee.
Vanessa Mdee.
Image: Insta

Aliyekuwa malkia wa Bongo Fleva Vanessa Mdee kwa mara ya kwanza amefunguka kuhusu safari yake ndefu na ngumu ya kuwalea wanawe wawili ambao aliwapata kwa mfululizo wa chini ya miaka miwili.

Mssanii huyo ambaye amepoa kimuziki tangu alipozama kwenye huba la msanii na muigizaji wa Marekani mwenye usuli wa Nigeria, Rotimi na hata kuhamia Marekani kabisa, alisimulia hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kwamba huku nje ni rahisi sana mtu kuona mama akiwa ametabasamu na wanawe mikononi lakini ni vigumu kuelewa safari ndefu na ngumu ambayo anapitia mpaka kuwakuza watoto hao.

Moja ya changamoto ambazo Mdee aliitaja katika kuwalea watoto wake ni kutolala hadi usiku wa manane kwa ajili ya kujaribu kumbembeleza mtoto kulala, kukosa kula kwa sababu ya kutumia muda mwingi kumlea mtoto na kujisahau kama ulihitajika kula miongoni mwa majanga mengine.

“Mpaka pale utakapokuwa mama, hakuna mtu ambaye anaweza kuelewa kile ambacho kuwa mama kinajumuisha. Kuchelewa kulala, kuamka mapema, kukosa kula yote kwa sababu uko bize kuwahudumia watoto wako. Iwe una msaidizi ama hapana, kazi ya mama ya mama haiwezi kukamilika,” Vanessa Mdee alisema.

 Msanii huyo alisema kwamba ndio maana kina mama wengi wanajisahau na kuja kugundua kwa kuchelewa kwamba walishakumbwa na matatizo ya unyongovu na msongo wa mawazo kutokana na kutumia muda mwingi katika kuwahudumia watoto na si kujihudumia wenyewe.

“Hakuna mtu anaelewa ujasiri na ukakamavu wa kiakili ambao unahitaji wakati linakuja suala la kuwa mama. Kukosa kupumzisha akili yako kwa sababu iko kazini usiku na mchana. Kuwa mama ni kazi 100 ndani ya moja,” aliongeza.

Mdee alitumia fursa hiyo kutoa ujumbe wa himizo kwa kina mama wengine ambao wanahisi kuchoka kwa malezi.

“Kwa kina mama wote ambao wanataabika wakijaribu kutafuta Amani na kupitia kwa mambo yote, kumbuka tu kwamba yeye ni kina mama bomba,” Vanessa Mdee aliandika.