Inawauma kuona nimedumu na Diamond mpaka leo - Zuchu awajibu wanaoonea penzi lake gere

"Watu vwengi wanasubiri tuachane ili waweze kufurahia," Zuchu.

Muhtasari

• “Inawauma sana watu, wanaangalia labda kwa nini mimi na mwenzangu [Diamond Platnumz] tumedumu mpaka sasa hivi," - Zuchu.

Image: Zuchu-Mungu anamtumia Diamond kama daranja ya mafanikio kwa wengi

Baada ya walimwengu kusema ya kwao kuhusu penzi la Zuchu na Diamond kufuatia msanii huyo bosi wa WCB Wasafi kuonekana na ukaribu wa aina yake na mama mtoto wake kutoka Kenya, Tanasha Donna, Zuchu hatimaye amevunja ukimya.

Zuchu katika mahojiano na Wasafi FM kwenye kipindi cha Refresh, alisema kwamba wengi ambao walionekana kufurahia kitendo cha Tanasha kuonekana na Diamond na kuhisi kwamba Zuchu muda wake ulikuwa umekwisha, ni wale wenye gere.

Zuchu anahisi kwamba wengi wanaofurahia kuona akipigwa figisu na kuchafuliwa kwenye penzi lake na Diamond ni wale wanaoumia ndani kwa ndani kwamba penzi lao limeweza kudumu kwa muda mrefu bila kuachana.

Zuchu alisema kwamba anaelewa fika kuwa kuna mahasidi wengi ambao wameketi pembeni na wanasubiria tu kitu kidogo kitokee ili wapaze sauti zao za shangwe kwamba ameachwa na Diamond, jambo ambalo hata hivyo alisema kwamba halitokuja kutokea na wanaosubiri bora wanajishughulishe na mengine.

“Inawauma sana watu, wanaangalia labda kwa nini mimi na mwenzangu [Diamond Platnumz] tumedumu mpaka sasa hivi, kwa hiyo wanasubiria kitu kidogo tu kikitokea hata cha uongo na kweli wakitengeneze kiwe kwa ukubwa huo. Lakini yaani kuna muda mwingine vitu vinaendelea watu wanakutafuta kukupa pole, ni vitu vya kawaida watu wa mitandaoni wanapenda kuzungumza,” Zuchu alisema pia akijibu kitendo cha mamake Diamond kuacha kumfollow Instagram.