Kutozwa ushuru kupita kiasi kunapunguza matumizi - Boniface Mwangi

Mwangi alisimulia hadithi ya rafiki aliyekuwa akienda nyumbani kila wikendi wakati petroli ilikuwa bei nafuu lakini akaacha kwenda kutokana na ughali wa petroli.

Muhtasari

• Kwa mujibu wa EPRA, bei ya mafuta ya petroli iliongezeka tena kwa Zaidi ya shilingi 5 kwa lita kutoka wastani wa shilingi 211 jijini Nairobi hadi shilingi 217.

Boniface Mwangi.
Boniface Mwangi.
Image: Facebook

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi ametoa hoja yake akihisi kwamba jinsi ambavyo serikali ya Kenya inatoza ushuru katika kila kitu kupita kiasi, hali hiyo imewafanya Wakenya wengi wamekoma kufanya matumizi ya hela zao.

 Mwangi anahizi kutozwa ushuru kupita kiasi hupunguza matumizi ya watu, kwani wengi wamelazimika kuweka pembeni baadhi ya vitu ambavyo wanaviona si vya lazima na hivyo biashara nyingi zimeathirika.

Akitolea mfano, Mwangi alitoa simulizi la rafiki yake ambaye siku za nyuma wakati kulikuwepo na unafuu wa hali ya uchumi nchini, alikuwa anakwenda nyumbani kijijini kila wikendi kwa ajili ya kukaa na wazazi wake wakongwe.

Mwangi alisema rafiki huyo alikuwa anatumia mafuta ya petroli ya shilingi elfu 6 kwenda na kurudi lakini tangu uchumi udorore na bei ya mafuta kuongezeka, alijipata analazimika kutumia mafuta ya shilingi elfu 10, hivyo kuifanya iwe vigumu kwake kuendelea na safari zake za kila wikendi kwa wazazi wakongwe nyumbani.

“Rafiki yangu alikuwa akiendesha gari hadi kijijini kila wikendi, ili kujumuika na wazazi wake wazee. Gharama yake ya mafuta ilikuwa Ksh 6,000 kwa safari ya kwenda na kurudi, kutokana na ongezeko la bei ya petroli, sasa ni Ksh 10,000, na ameacha kwenda kijijini kila wikendi. Kutozwa ushuru kupita kiasi kunapunguza matumizi!” Mwangi alisema.

Ni hivi majuzi tu ambapo mamlaka ya kudhibiti bei za bidhaa za kawi EPRA ilitangaza bei mpya za mafuta katika kipindi cha siku 30 zijazo.

Kwa mujibu wa EPRA, bei ya mafuta ya petroli iliongezeka tena kwa Zaidi ya shilingi 5 kwa lita kutoka wastani wa shilingi 211 jijini Nairobi hadi shilingi 217.

Waziri wa kawi Davis Chirchir akitokea mbele ya kamati ya bunge, alitetea bei hizo mpya akisema kwamba kusingekuwa na ruzuku ya serikali , bei hiyo ingeongezeka kwa hadi shilingi 8, akisema kuwa ni hali ilivyo sit u humu nchini bali pia katika rubaa za kimataifa.