Pasta Ng'ang'a afichua sababu ya kuchukia watu wa digirii kuhudhuria mahubiri yake

"Na wale watu wameharibu dunia nzima ni wasomi, nyinyi ndio mmeleta wanaume walalane, na mkapitisha kortini, na hiyo yes yes yes zenu,” Ng’ang’a alisema.

Muhtasari

• Hii ni baada ya majaji wa mahakama ya upeo kupitisha uamuzi wa kuhalalisha makundi ya LGBTQ nchini Kenya kuwa na uhuru wa kujumuika.

Pasta Ng'ang'a
Pasta Ng'ang'a
Image: TikTok//Screengrab

Siku chache zilizopita, mchungaji mwenye utata kutoka kanisa la Neno Evangelical, James Ng’ang’a aligonga vichwa vya habari kwa kuonesha hadharani chuki na kero lake dhidi ya wasomi wenye vyeti vya shahada kuhudhuria mahubiri katika kanisa lake.

Mchungaji huyo sasa ametoa ufafanuzi Zaidi kuhusu chuki hiyo akisema kwamba dunia nzima imeharibiwa katika kila mifumo sahihi ya kimaadili ya watu ambao wanajiita ni wasomi.

Ng’ang’a alisema kwamba wanaojidai kuwa wasomi wenye maarifa yenye haiba zilizotukuka ndio hao hao ambao wanashinikiza kuhalalishwa kwa jumuiya za LGBTQ miongoni mwa mambo mengine aliyoyataja kama ya ajabu hata mbele ya macho ya Mungu.

“Na wale watu wasomi, tafahdali tuheshimiane, Daudi si msomi, hata wale mitume amechagua wote maandiko yanasema hawakuwa wasomi. Na wale watu wameharibu dunia nzima ni wasomi, nyinyi ndio mmeleta wanaume walalane, na mkapitisha kortini, na hiyo yes yes yes zenu,” Ng’ang’a alisema.

Mchungaji huyo alikwenda mbele akisema kwamba hata wanyama mbwa wanaodharauliwa wamewashinda wasomi kimaadili licha ya kujifanya kuwa wanajua sheria.

Hii ni baada ya majaji wa mahakama ya upeo kupitisha uamuzi wa kuhalalisha makundi ya LGBTQ nchini Kenya kuwa na uhuru wa kujumuika.

“Na mbwa wa kiume halali na mbwa mwenzake wa kiume, sasa mnakuja hapa kusema eti yule mhubiri hana masomo eti hawezi kuhubiri Kenya, aje? Yaani mkikaa tu ni wale watu hawajasoma mnaona, tumewazuia nini? Tunawaoshea vyoo, tunafanya kazi kwa nyumba zenu sisi ambao hatukusoma, tunawapelekea pesa benki, sasa mpaka kanisani mnatukandia,” Ng’ang’a aliongeza.

Alisisitiza kwamba hakuna mahali imeandikwa kwamba ni lazima Mungu aongee au kuongeleshwa kwa Kiingereza.