H_Art the Band, Wanavokali, Vijana Barubaru... Bendi zinazopigiwa upato kurithi Sauti Sol

Sauti Sol walitangaza kuvunja bendi yao kwa muda, baada ya shoo yao ya mwisho wikendi iluyopita. Hii ni baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka 18.

Muhtasari

• Maoni yako ni yepi kuhusu mrithi halisi wa Sauti Sol kama bendi yenye ushawishi mkubwa kimuziki nchini?

Sauti Sol wakiwasha nchini Uganda katika tamasha la Boyz ii men.
Sauti Sol wakiwasha nchini Uganda katika tamasha la Boyz ii men.
Image: RADIO AFRICA EVENTS

Wikendi iliyopita, bendi marufu ya muziki wa sekula kutoka humu nchini, Sauti Sol walihitimiza kile walichosema ni safari yao ya karibia miaka 20 pamoja kwa kufanya shoo fungakazi.

Sauti Sol walifanya shoo hiyo katika ukumbi wa Uhuru Gardens na kuwapa mashabiki wao burudani la mwisho wao kuonekana pamoja wakitarajiwa kila mmoja kujishughulisha na hamsini zake katika Sanaa.

Hata hivyo, si mara moja bendi hiyo wamesisitiza kwamba kufanya kwa shoo ya mwisho si mwisho wao kabisa bali ni mapumziko ya muda ambapo kila mmoja anatathmini safari yake binafsi na kama nafasi itajipa mbeleni basi wataungana tena kuachia nyimbo kwani kila mmoja kwenda kivyako si mwanzo wa uadui.

Wakati Sauti Sol wanatawanyika, Wakenya katika mitandao ya kijamii wamezua maswali mengi kuhusu ni bendi gani nyingine ambayo inakaribia kuliziba pengo linaloachwa na Sauti Sol baada ya kuwa katika kilele cha muziki wa Kenya kwa miaka 18.

Katika mjadala huo, baadhi ya bendi zilitajwa kuwa na uwezo wa kujaribu angalau kuziba pengo hilo japo ni vigumu kuliziba kabisa lakini kwa kujaribu tu.

H_Art the Band.

Hii ni bendi ya muda mrefu inayowajumuisha vijana watatu ambao wameuweka muziki wa Afrika Mashariki katika ramani ya dunia, mara nyingi wakitajwa kuwa walikuwa wanafuata nyayo za Sauti Sol.

Wasanii hawa watatu mahiri Mordecai Mwini Kimeu, Wachira Gatama na Kenneth Muya Mukhwana wamekaidi vikwazo vyote dhidi yao kutajwa kuwa moja ya bendi bora nchini Kenya na Afrika Mashariki.

Wanavokali.

Wanavokali ni bendi ya vijana wadogo ambayo ilijipatia umaarufu miaka michache iliyopita baada ya wimbo wao wa ‘Rhumba’ wa mwaka 2021 kushabikiwa kama utunzi bora nchini na kuwapa umaarufu kama moja ya bendi inayokua kwa kasi nzuri kwenye tasnia ya muziki Kenya.

Wanavokali ni kundi la wanamuziki sita wa Kikenya Chep, Lena, Mella, Riki, Sam, na Ythera. Wanashiriki shauku ya kujieleza kupitia muziki na kuona tasnia ya muziki nchini Kenya ikiimarika na kuwa bora zaidi.

Vijana Barubaru.

 Ndio kundi la tatu ambalo lilipata kutajwa kwa wingi kama warithi wa Sauti Sol katika muziki wa kizazi kipya Kenya.

V-Be maarufu kwa jina la Vijana Barubaru wametamba na kupokelewa kwa mbwembwe ikiwa ni muda mfupi tu ambao wamekuwa kwenye tasnia ya muziki wa Kenya. Ni bendi ambayo inatajwa kuimba muziki unaoashiria taswira halisi ya utamaduni wa Kenya.

Vijana Barubaru ndio waundaji wa Sasa Hivi, wimbo maarufu wa mapenzi wa R&B ambao kwa sasa unavuma kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya kutiririsha muziki.

V-BE ni bendi ya wanamuziki wawili, Mshairi Spikes, rapa mwenye ushawishi mkubwa kwenye ushairi, na Tuku Kantu, mwimbaji mahiri na mwenye ushawishi mkubwa kwenye muziki wa pop.

Wakadinali.

Kundi hili pia limekuwa kwenye tasnia kwa muda kiasi na wamepata umaarufu mkubwa kutokana na rap inayohusishwa na muziki wa gengetone.

Wakadinali pia wanajulikana kama Rong Rende ni kikundi cha muziki cha Kenya kilicho katika eneo la Eastland Nairobi.

Kikundi kinaangazia aina ya muziki wa Hip-Hop. Wakadinali inaundwa na vijana watatu ambao ni; Scar, Domani na Sewersydaa.

Scar na Domani ndio waanzilishi wakuu. Wawili hao walisoma pamoja na walianza mwaka wa 2003 kabla ya baadaye kuunganishwa na Sewersydaa.

Maoni yako ni yepi kuhusu mrithi halisi wa Sauti Sol kama bendi yenye ushawishi mkubwa kimuziki nchini?