Justina Syokau aweka bango akitafuta kijana bilionea wa 'kupanda miti na yeye'

"Niko soko tayari kuolewa kabla ya 2024, vigezo ni kwanza uwe bilionea na pili uwe wa miaka 25,” bango hilo lilisoma.

Muhtasari

• “Ni wapi mabilionea wanaishi Kenya Nipeleke soko huko? Ni sharti nipate bilionea, kwa nguvu zote hakuna kulala.”

Justina Syokau
Justina Syokau
Image: Facebook

Msanii wa injili Justina Syokau amezua gumzo mitandaoni baada ya kuonekana katikati mwa jiji la Nairobi akiwa anazunguka na bango lenye matakwa ya mwanamume ambaye anamtafuta kuazna maisha ya uchumba pamoja.

Justina kupitia ukurasa wake wa Facebook alipakia video na picha akiwa amebeba bango msobe msobe lenye maandishi ya matakwa ya mwanamume ambaye angependelea kumpata.

Katika bango hilo, Justina anaweka wazi kwamba kigezo cha kwanza cha mwanamume anayemtaka ni sharti awe tajiri wa kiwango cha ubilionea na pili sharti awe na miaka 25 tu.

Justina alisema kwamba msimu huu wa mvua za masika, angependa kupata kijana huyo ili wakashirikiane katika shughuli ya upanzi wa miti ambayo ilizinduliwa rasmi Novemba 13 na rais Ruto – siku ambayo ilitajwa kama likizo ya kupanda miti kote nchini.

“Natafuta bilionea wa kupanda miti twende tukapande pamoja,” Justina aliandika kwenye picha akiwa na bango.

Msanii huyo alisema kwamba azma lake kuu ni kupanda mchumba na kuolewa kabla ya mwaka ujao huku akiweka bayana kwamba kwa sasa yuko sokoni na anamtafuta bilionea.

“Niko soko tayari kuolewa kabla ya 2024, vigezo ni kwanza uwe bilionea na pili uwe wa miaka 25,” bango hilo lilisoma.

Akiwa katika mizunguko naye mjini na bango, Justina alikuwa anauliza ni sehemu gani ya Nairobi ambapo mabilionea wanaishi akisema kwamba ni sharti angejipeleka huko akisisitiza kwamba inyeshe mvua liwake jua, lazima angepata mpenzi tajiri.

“Ni wapi mabilionea wanaishi Kenya Nipeleke soko huko? Ni sharti nipate bilionea, kwa nguvu zote hakuna kulala.”