Tuzo alizopewa Harmonize ni feki, Baba levo adai

Baba Levo, amechana Harmonize akisema kuwa tuzo alizozipata ni za kitoto.

Muhtasari

•Harmonize alishinda tuzo 3 kwa kuwabwaga wasanii wakubwa wa Afrika katika tuzo za African Entertainment Awards.

Harmonize na Baba Levo.
Harmonize na Baba Levo.
Image: Instagram

Msanii wa Tanzania, Revokatus Kipando, almaarufu Baba Levo, amechana msanii Harmonize akisema kuwa tuzo alizozipata ni feki na za thamani ya chini.

Baba Levo alisema hayo kwenye mahojiano ya moja kwa moja na wanablogu.

"Zile tuzo anayeshangilia ni Harmonize peke yake hata hakuna msanii mwingine ameziweka kwenye mitandao, kwa maana ni tuzo ndogo sana kama zile zinapeanwa kwa mashindano ya kanisa,"alisema Baba Levo.

"Sisi hatuwezi kushabikia tuzo za kitoto kama hizo, ndio maana wasanii wamengudua ni za chini hakuna aliyeziposti",alisema.

Baba levo amechana Harmonize siku chache baada  ya kushinda tuzo tatu kwa mpigo katika hafla iliyoandaliwa nchini Marekani.

Harmonize alishinda tuzo tatu kwa kuwabwaga wasanii wakubwa wa Afrika katika tuzo za African Entertainment Awards.

Tuzo ya kwanza aliyoshinda kwa kura nyingi ni tuzo ya msanii bora wa mwaka barani Afrika, akashinda pia video bora ya mwaka kupitia ngoma yake ya Single Again na pia akatajwa kama mfalme wa muziki wa Afrika Mashariki na Bongo Fleva kwa jumla.

Katika tuzo hizo, Harmonize aliwaonyesha kivumbi wasanii kama vile Libianca kutoka Cameroon ambaye amekuwa akifanya vizuri, Asake, Burna Boy, Davido, Tiwa Savage, Yemi Alade, Rema wote kutoka Nigeria na Diamond Platnumz kutoka nyumbani Tanzania.