Aliyenipa mimba aliniacha na kuoa mke mwingine nikiwa na ujauzito wa miezi 5 - DJ Pierra Makena

"Hakuwa mwanamume aliyekuwa kwenye ndoa tukioana, tulichumbiana kwa muda mrefu na tukaachana wiki mbili baadae ndio niligundua niko na mimba yake,” alisimulia.

Muhtasari

• "Tulikuwa na uhusiano mzuri sana, lakini wakati nilipata ujauzito na tukaachana, aliondoka" alisema Makena.

• Mrembo huyo alifichua sababu ambayo inamfanya kutopenda kumzungumzia baba mtoto wake.

DJ Pierra Makena
DJ Pierra Makena
Image: Instagram

Mcheza Santuri Pierra Makena kwa mara ya kwanza amefungulia mwanga japo kwa kiduchu kuhusu mwanamume ambaye walikuwa na uhusiano na yeye na kupata mtoto mmoja.

Makena ambaye ni mama wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 7 sasa amefichua kwamba baba wa mtoto wake alimuacha pindi tu baada ya kupata mimba na miezi mitano baadae, mwanamume huyo alifunga harusi na mwanamke mwingine – kipinndi hicho Pierra akiwa na mimba ya miezi 5.

DJ huyo maarufu alisema kwamba mwanamume huyo alimtelekeza yeye na mwanawe tangu wakati huo lakini akaapa kwamba hakuna hata siku moja ataelekea mahakamani kumshurutisha baba mtoto wake kujukumikia malezi ya mtoto.

“Mwenyewe nilijiaminisha wakati niligundua kwamba niko na mimba na mhusika asingeweza kuhusika moja kwa moja. Tulikuwa na uhusiano mzuri sana, lakini wakati nilipata ujauzito na tukaachana, aliondoka. Hakutaka kitu chochote kuhusu na sisi, na alinyoosha maelezo kuhusu hilo, hakuleta drama wala kunitukana, hapana. Lakini miezi mitano baadae nikiwa na mimba, alioa mwanamke mwingine,” Makena alisema.

Mrembo huyo ambaye alifutilia mbali uwezekano wa kupata mtoto mwingine alisema kwamba kipindi hicho cha kuachwa na mpenzi wake kuoa miezi 5 tu baadae kilimuuma sana kiasi kwamba hakuwahi kufikiria angeweza kujikusanya pamoja tena na kuanza upya.

“Hiyo ilikuwa ya kuvunja moyo sana, sikuwahi fikiria ningeweza kujiweka pamoja na kusahau tukio hilo lakini niliweza. Nilifurahia kwake kwa sababu nilihisi alipata furaha yake. Na hiyo ndio maana mimi siwezi chunguza wala kufuatilia maisha yake. Hakuwa mwanamume aliyekuwa kwenye ndoa tukioana, tulichumbiana kwa muda mrefu na tukaachana wiki mbili baadae ndio niligundua niko na mimba yake,” alisimulia.

Mrembo huyo alifichua sababu ambayo inamfanya kutopenda kumzungumzia baba mtoto wake.

Pierra alisema kwamba huyo kwa sasa ni mume wa mtu ambaye ana watoto na familia na asingependa kuharibu ndoa yake kwa kulivuta jina lake katika songobingo la mitandaoni.