Kipenzi cha Diamond Platnumz ambaye pia ni chawa mtunza siri mkubwa wa WCB Wasafi, Baba Levo ametoa tamko la ushauri wenye mkwara mzito kwa sajili mpya wa WCB, D Voice, saa chache tu baada ya kutambulishwa.
Baba Levo katika video fupi aliyopakia kwenye ukurasa wake wa Instagram alimshauri dogo D Voice kuzingatia heshima na taratibu zote kwa kuzingatia kwamba familia ya Wasafi imempokea akiwa maskini.
Baba Levo alisonga mbele kufichua kiasi cha hela ambacho wamemsajili msanii huyo nacho na kumtaka kuepuka kabisa mtihani wa kuingiwa na kiburi pindi mambo yake yatakaponyooka kwani kule Wasafi alikoingia kuna uhakika mkubwa wa mambo kumuendea vizuri, akiitaja lebo hiyo kama karakana na kunyoosha vitu na kuviweka katika hali sawa na kutamanika.
“Wewe D Voice, usije utugeuke wenzako tumeshawekeza hela ujifanye kama na wewe eti ‘mimi nilikuwa tajiri’ ulikuwa tajiri na wewe wapi. Ulikuja na elfu 60 tu,” Baba Levo alisema kwa sauti ya ulevi.
Levo aliweka utani pembeni na kumpa ushauri dogo huyo akimwambia kwamba Wasafi walimchagua kwa sababu waliona ana talanta kubwa na ndio maana watu wengi walijitokeza kusikiliza na kuhudhuria uzinduzi wake na albamu yake ya kwanza siku yake kuu usiku wa Novemba 16.
“Una talanta kubwa mwanangu, Mungu akujaalie. Una kipaji sana ndio maana wamekuja watu wengi. Kabla ya kuheshimu Wasafi wenyewe unatakiwa kuheshimu kipaji chako, cha pili mheshimu Mwenyezi Mungu na cha tatu heshimu Wasafi kwa namna ambavyo wamesapoti kipaji chako,” alisema.
DVoice ambaye ana kipaji kikubwa katika miziki ya Singeli ameingia kwenye vitabu kama msanii wa 7 kuwahi kusajiliwa na lebo hiyo inayomilikiwa na Diamond Platnumz na washikadau wengine.
Watangulizi wake ni kama Harmonize anayefanya vizuri tangu kuondoka Wasafi miaka 4 iliyopita, Rayvanny aliyeondoka mwaka jana, Queen Darleen, Mbosso, Zuchu, na Lava Lava ambao bado wapo chini ya lebo ya WCB Wasafi.