Riggy G na Karen Nyamu waonesha ustadi wa kucheza densi ya 'ruracio' mwendo taratibu

Wanasiasa hao walitimba kwenye dance floor wakati wa hafla ya kitamaduni ya kulipa mahari - Ruracio - ya wabunge wa UDA huko Murang'a.

Muhtasari

• Hafla hiyo ilikuwa ya mbunge wa Mathira Eric Wamumbi na mwakilishi wa kike kaunti ya Murang’a Betty Maina ambao ni wapenzi.

Karen Nyamu na Riggy G
Karen Nyamu na Riggy G
Image: Instagram

Seneta maalum Karen Nyamu hakosi kujipata katika vichwa vya habari kila uchao iwe kwa taarifa hasi au chanya.

Kwa mara nyingine tena Nyamu amegeuka gumzo la mitandaoni baada ya kupakia rundo la picha kutoka kwa tukio la hafla ya kitamaduni ya kulipa mahari – ruracio – ya wabunge wa chama tawala wa UDA iliyofanyika Jumamosi katika kaunti ya Murang’a.

Hafla hiyo ilikuwa ya mbunge wa Mathira Eric Wamumbi na mwakilishi wa kike kaunti ya Murang’a Betty Maina ambao ni wapenzi.

Katika tukio lao la kitamaduni, wanasiasa mbalimbali kutoka mirengo yote walihudhuria, lakini tukio ambalo limezua minong’ono mitandaoni ni lile la seneta Karen Nyamu akicheza densi na naibu rais Rigathi Gachagua, kwa jina la utani Riggy G.

Wakiwa wamevalia mavazi ya rangi ya chungwa iliyochuchumaa, Nyamu na Riggy G walitimba kwenye uwanja wa kusakata densi katika kile kilionekana kama ni kunengua kwa mwendo wa taratibu.

Seneta huyo alipakia picha hizo kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuvutia maoni mengi, baadhi wakimtania Samidoh – mpenzi  wake – kuwa asione hizo kwani atapatwa na wivu.

Haya hapa ni baadhi ya maoni ya wanamitandao;

“Samidoh Muchoki mimi nilikuambia Riggy G si mtu mzuri,” Kelvin Shaban alitania.

“Baada ya Gachagua kumwambia askari [Samidoh] apange watu wake kumbe ndio alikuwa anataka kumsaidia kupanga mmoja,” mwingine alitania.

“l told you mzee alienda Haiti, sasa ni kupiga sherehe na ujue Riggy G hatumi veve wala Jaba juice, ni mtu wa chai,” Mike Sonko alisema.