Jackson Mulai, maarufu kama J M ambaye ni muongozaji wa video za msanii Mbosso Khan katika lebo ya Wasafi WCB kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kufuatia tukio la siku chache zilizopita aliposhambuliwa na majambazi waliomchangara mapanga na kumuacha hoi.
Akizungumza na Wasafi FM kupitia njia ya simu, JM aliweza kusimulia jinsi matukio yalivyotukia siku ya msala na kusema kwamba vibaka hao walikuwa wanataka kumuibia begi lake ambalo lilikuwa na kipakatalishi pamoja na kamera mbili miongoni mwa vitu vingine vyenye thamani.
JM alivamiwa nyakati za saa tisa alfajiri alipokuwa akitoka kazini.
“Nilipata matatizo Jumatano kuamkia Alhamisi iliyopita siku ambayo tulikuwa tunatoka locations kushoot lakini kibaya zaidi siku hiyo mimi sikuwa na gari kwa hiyo nilikuwa natumia bodaboda tu. Ilikuwa ni mida ya saa tisa kuelekea saa kumi,” JM alisimulia.
“Njiani wakatokea watu sijui niseme vibaka au majambazi mmoja alikuwa ni dereva mwinigine alikuwa ameshika panga na wakatoka mbele yangu, wakafika pale kama wanataka kutugonga na kusimama mbele yetu. Hawakutaka kuuliza chochote, walitoa mapanga na kuanza kutupiga, walinicharanga panga la kichwani kwamba ‘toa begi, toa simu’”
“Pale mimi nikawa mbishi kidogo kwa sababu bego langu lilikuwa na kipakatalishi na kamera mbili. Nikawa nimekaza na dereva alivyoona nimepigwa panga akaruka na kuacha pikipiki hapo. Mimi pia nikaruka nikakimbia simu yangu nikiwa nimeshikilia mkononi,” alisema.
“Katika harakati ya kukimbia sikuelewa kilichofuata ila tu nilikuta bodaboda moja iliyokuwa imempakia dada na nikawasimamisha kuwaomba msaada ‘bwana naomba mnipeleke hospitali ninavuja damu’. Nilikuwa nimeshapigwa panga la shavuni na la mkononi ile kuzuia kupigwa kichwani,” JM aliongeza.
Hata hivyo, alisema kwamba majambazi wale walifanikiwa kuchukua simu moja iliyodondoka lakini hawakufanikiwa kuchukua begi lake lililokuwa na vyombo vyake vya kazini.
“Kwa sasa hivi naendelea vizuri, nashukuru menejimenti yangu na kila mtu ambaye alisimama upande wa faraja yangu, lakini pia ningependa kutoa angalizo kwa vijana wenzangu ambao tunahangaika kutafuta, tuwe makini sana nyakati za usiku,” alisema.