Msanii Harmonize ameanza kwa kishindo kikuu kuitangaza albamu yake ijayo, Visit Bongo.
Katika mahojiano yake na kipindi cha XXL ndani ya stesheni ya Clouds, Harmonize aliweza kufunguka kuhusu ngoma za wasanii wengine wa Bongo Fleva ambazo anazikubali kando na zile za kwake.
Katika orodha ya ngoma 10, Harmonize aliweka wazi kwamab ana mapenzi makubwa kwa ngoma za wasanii wa WCB Wasafi, licha ya kwamba yeye na bosi wa lebo hiyo pinzani, Diamond Platnumz hawaonani jicho kwa jicho.
Harmonize alisema kwamab anaipenda pakubwa ngoma ya Mbosso – Sele akisema kuwa inamkumbusha ngoma za kizamani ambayo walikuwa wanaiskiliza wakiwa vijana.
“Ninapenda nyimbo nyingi mpaka zingine zinanichanganya, Sele ya Mbosso naipenda sana, inanikumbusha enzi za mtoto Idd kazua balaa, yaani vaibu kama hiyo tukiwa shule. Nikisikiliza hiyo naona vizuri kabisa kwamba ni ngoma nzuri,” Harmonize alisema akijaribu kuimba ngoma hiyo.
Lakini pia alionesha mapenzi makubwa kwa Zuchu – mpenzi wa mabanoni wa Diamond Platnumz akitaja ngoma yake mpya ya ‘Naringa’ kama moja ambayo inamkosha sana.
Harmonize alikiri kwake kwa tathmini yake, ngoma ya ‘Naringa’ ndio bora Zaidi kuwahi kutoka kwa Zuchu tangu aanze kuimba, akionekana kuifutilia mbali ile ya ‘Sukari’ ambayo wengi wanahisi ndio ilimpa umaarufu mkubwa Zuchu mwaka 2020 kipindi hicho watu wakiwa majumbani kwa kuhofia janga la Covid-19.
“Zuchu ile yake ya ‘Na ndio maana naringa’ nadhani ndio moja ya ngoma nzuri ambazo amewahi kuwa nazo. Kwa mimi shabiki wa huo wimbo nadhani kwamba ndio wimbo wake bora tangu aanze kuimba,” alisema Harmonize.
Msanii huyo wa Konde Gang alisema kwamba nyakati ambazo anasikiliza ngoma za wasanii wengine kando na wale wa Konde Music Worldwide ni wakati anaendesha gari, akiwa gym lakini pia muda mwingi akiwa ametulia mwenyewe.