Eric Omondi atoa sababu kwa nini hajasaidia Magix Enga na Mwana Mtule

hata hivyo Omondi alizungumzia swala hilo, akieleza kuwa alihitaji muda zaidi wa kuelewa hali ya Mwana Mtule kabla yakushauri umma kumuunga mkono.

Muhtasari

• Licha ya kuchangisha pesa kwa ajili ya Wakenya wengine wanaotatizika, ukimya wa Eric Omondi kuhusu hali ya rafiki yake wa karibu Mwana Mtule umeibua sintofahamu 

• "Bado natafuta kilichompata kabla sijarudi na kuwaambia Wakenya wamuunge mkono."

Mcheshi na Mwanaharakati Eric Omondi
Mcheshi na Mwanaharakati Eric Omondi
Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi amejipata katika njia panda baada ya kususia kujitokeza kumsaidia mwanamuziki wa Injili anayeugua, Alpha Mwana Mtule, ambaye amekuwa akipambana na masuala ya kiafya kwa takriban mwezi mmoja.

Licha ya kuchangisha pesa kwa ajili ya Wakenya wengine wanaotatizika, ukimya wa Eric Omondi kuhusu hali ya rafiki yake wa karibu Mwana Mtule umeibua sintofahamu na kuzua wasiwasi miongoni mwa Wakenya.

hata hivyo Omondi alizungumzia swala hilo, akieleza kuwa alihitaji muda zaidi wa kuelewa  hali ya Mwana Mtule kabla yakushauri umma kumuunga mkono.

“Mwanzo wa simulizi hii ilipotoka nilikuwa naelekea Meru, nikaona stori inayotrend kuwa Mwana Mtule amefariki ndipo nikasoma anakaribia kutoa albamu. Kisha mke wake akanipigia simu baadaye, akaniambia kuwa aliwekewa sumu huko Rongai. Sikujua hadithi haswa. Bado natafuta kilichompata kabla sijarudi na kuwaambia Wakenya wamuunge mkono. Sitaki kushambuliwa kwenye mitandao ya kijamii,” Eric Omondi alieleza.

Aidha alisisitiza haja ya kuangalia kwa kina hali za wasanii wanaohangaika kama vile Mwana Mtule na Magix Enga kabla ya kuanza jitihada za kutafuta fedha.

"Sababu ya kutochangisha fedha kwa ajili ya wasanii wawili wa sasa ambao wanahangaika, Magix Enga na Mwana Mtule, ni kwa sababu nahitaji kufanya uchunguzi wa kina ili kujua nini kinatokea," aliongeza.

Kuhusu kesi ya Magix Enga, ambaye hivi majuzi aliomba kuungwa mkono kutokana na matatizo ya kifedha, Eric Omondi alieleza wasiwasi wake kuhusu uaminifu wa ombi hilo, akizingatia kauli za awali zilizotolewa na Magix Enga.

“Niliangalia kwa mfano katika suala la Magix Enga kuna wakati alisema yeye ni Illuminati akasema kuna fedha. Je, nije tena na kuwaambia Wakenya kwamba mtu huyu anahitaji usaidizi? Wakenya hawatanisikiliza nitakapotaka msaada wao,” Eric Omondi alisema.

Licha ya Eric kususia kwa swala hilo  alitoa wito adimu wa kuwepo wa umoja miongoni mwa wasanii wa Kenya ili kumuunga mkono Mwana Mtule hasa wakati huu anapopitia hali ngumu.

“Kwa Mwana Mtule, nitoe wito kwa wasanii wote wakiwemo ma-DJ na wachekeshaji kuungana na kuchangisha fedha za matibabu. Sisi kwa Sisi kama Wasanii manake hili linahusu wasanii. bili yake ya hosipitali ni ndogo zaidi  kwa wasanii wote kukusanyika na kumuunga mkono kama mmoja wao,” Eric Omondi alihimiza.