Mimi ni risk-taker na nimetengeneza wasanii wengi mamilionea - Diamond Platnumz

Kwa kurudisha akrabu ya saa nyuma, Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kuchuma martunda ya kusainiwa kwenye lebo ya Wasafi mwaka 2015 hata kabla ya lebo hiyo kusajiliwa rasmi.

Muhtasari

• Diamond ni mmoja wa watu waliowekeza pakubwa kwenye biashara ya muziki kwa kusaini wasanii na ambaye amevuna pakubwa.

Wasanii wa WCB Wasafi siku za nyuma.
Wasanii wa WCB Wasafi siku za nyuma.
Image: Screengrab// Wasafi

Mkurugenzi wa lebo ya muziki ya WCB Wasafi, Diamond Platnumz amefunguka kwamba yeye ni mmoja wa watu wana uwezo wa kuchukua maamuzi hatari kwa lengo ya kufanikiwa kutokana nayo mbeleni, ambaye amefanikiwa pakubwa katika hilo.

Diamond kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika kwamba yeye ni mmoja wa watu waliofanya maamuzi magumu kama hayo na kuwekeza kwenye lebo wakati ambapo wengi waliona sekta hiyo kama kupanda mgomba wa ndizi kwenye changarawe.

Lakini kwa kuangalia nyuma miaka 8 iliyopita tangu kuzindua rasmi WCB Wasafi, Diamond ni mjasiriamali wa kujivunia, akisema kwamba kupitia kwa wazo lake hilo, amewaibua wasanii wengi ambao wanafanya vizuri, akikisia kwamba baadhi utajiri wao umevuka kiwango cha bilioni za nchini Tanzania.

“Utajiri wa kizazi kwenda kizazi kingine huanza na risk taker mmoja. Mimi ni mmoja wa risk takers hao. Angalia sasa ni mabilionea wangapi wachanga ambao nimetengeneza, angalia ni mamilionea wangapi tasnia ya muziki imetengeneza. Inaitwa mapinduzi,” Diamond aliandika huku akimalizia na alama ya reli na neno Wasafi.

Kwa kurudisha akrabu ya saa nyuma, Harmonize alikuwa msanii wa kwanza kuchuma martunda ya kusainiwa kwenye lebo ya Wasafi mwaka 2015 hata kabla ya lebo hiyo kusajiliwa rasmi.

Kupitia kwa lebo hiyo, ndani ya miaka 4 tu mpaka kuondoka kwake, msanii huyo alikuwa jina kubwa kiasi kwamba alipoondoka tu alianzisha lebo yake ya Konde Music Worldwide na mpaka sasa anazidi kufanya vizuri.

Msanii wa pili, Rayvanny ambaye pia ameondoka Wasafi mwaka jana baada ya miaka kama 6 kwenye lebo alianzisha lebo yake ya Next Level Music na kusajili msanii Macvoice ambaye anapigiwa upato kufanya vizuri.

Lakini pia wasanii wengine kama Lavalava, Mbosso na Zuchu ni wasanii wa kutajika ambao wamejizolea utajiri mkubwa kutokana na muziki, shukrani kwa lebo ya Wasafi.

Msanii wa hivi karibuni, Dvoice naye anapigiwa upato kuinukia na kuwa jina la kaya kwa ujio wake ambapo alitambulishwa na albamu yake ya Swahili Kid ambayo imepata mapokezi ya kuridhisha mpaka sasa wiki mbili.