Gwiji wa Rhumba kutokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide hatimaye ametua nchini Kenya baada ya kusubiriwa kwa miaka mingi kufanya urejeo wako.
Msanii huyo ambaye yuko nchini kwa ajili ya shoo ya kipekee ya Koffi Olomide Peace Concert ambayo imeafadhiliwa na Radio Africa Group baada ya kutua, alijawa na furaha mpaka kukosa maneno ya kueleza jinsi alivyojihisi kuingia nchini.
Olomide alisema kwamba ana furaha kubwa kurudi Kenya tena ikiwa ni Zaidi ya miaka 7 iliyopita alipopatwa na kashfa ya kumsukuma mrembo mcheza densi kwenye jukwaa.
Aliomba nafasi ya kufikiria cha kusema kabla ya kuzungumza kutokana na furaha ghaya aliyokuwa nayo kureja tena kwa ‘ndugu zangu wa kenya’.
“Jinsi ninavyohisi? Nipe muda wa kufikiria, nina furaha Zaidi, nimerejea kupanda jukwaani tena, kukutana na mashabiki wangu, watu wa Kenya ambao ninawapenda sana, nimewakosa kwa muda mrefu. Sijui jinsi mtu kama mimi ninaweza kuhisi baada ya muda mrefu, nina furaha sana furaha kubwa sana,” Olomide alisema.
Pia aliimiminia sifa serikali mpya ambayo alidokeza ilifanya mchango mkubwa kwa kuondolewa kwa marufuku yake kufuatia tukio lile la 2016 akimsukuma mrembo jukwaani.
“Kwanza kabisa shukrani sana kwa uongozi mpya, rais na watu wote wa Kenya, hapa ninahisi kama niko nyumbani, ni nchi yangu hii na ya moyo wangu, nina historia ndefu ya maisha yangu hapa na kurejea baada ya miaka mingi, jaribu kunielewa, ni kitu ambacho kimekuwa katika moyo wangu,” alisema.
Shoo ya Koffi Olomide itafanyika Jumamosi Desemba 9 katika uwanja wa ASK Dome Jahmuri katika barabara ya Ng’ong jijini Nairobi.