Kiungo wa kati wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana na vilabu kama vile Real Madrid, AC Milan, Chelsea miongoni mwa vingine, Michael Essien amemsifia msanii wa Bongo, Harmonize kwa njia ya kipekee katika kile alikitaja kuwa anafanya mambo makubwa kimuziki.
Essien alikuwa anasherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo alipakia picha yake kwenye ukurasa wake wa Instagram huku akionesha kufurahia wimbo wa Harmonize ‘Sijalewa’.
Essien, raia wa Afrika Magharibi aliwashangaza wengi wa kukumbatia wimbo wa Harmonize ambao umetungwa kwa lugha ya Kiswahili, licha ya kwamba yeye [Essien] hajui Kiswahili hata kidogo.
Baada ya kuonesha heshima hiyo kubwa kwa wimbo wa Harmonize, msanii huyo alifika kwenye ukurasa wake na kumuandikia ujumbe mrefu wa kumshukuru huku pia akifichua kwamba kitambo akiwa Chelsea, yeye [ Harmonize] alikuwa anafuatilia mchezo wake kwenye runinga za vibandani na kumfanya kipenda Chelsea.
“happy birthday kwa Jamaa aliyebadili ndoto yangu kutoka ⚽️ kwenda muziki love you g @michaelessien nakumbuka jinsi nilivyotumia usafiri 2 kutoka kijiji kimoja hadi kingine ili kutazama @chelseafc my first love club !!!!! 😢😢😢😢umefanya hivyo 🙌🙌🙌 mapenzi kubwa nahodha wangu ❤️⚽️” Harmonize aliandika.
Kwa upendo wa ajabu, Essien alimjibu akisema kwamba muziki ni lugha ya kidunia ambayo inasikika na moyo tu hata kama mtu hana weledi wa kile kinachoimbwa.
Mchezaji huyo wa zamani ambaye sasa hivi ni mkufunzi alimwambia Harmonize kwamba anafanya kazi kubwa kimuziki na kumtaka kuendelea vivyo hivyo.
“Unachokifanya na muziki ni cha ajabu sana, endelea hivyo kaka Harmonize, upendo mkubwa,” Essien alijibu.
Itakumbukwa Essien si mchezaji wa kwanza kufagilia ngoma za Harmonize.
Wiki mbili zilizopita mchezaji wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni alisifia wimbo wake wa Single Again akisema kwamba ni moja ya nyimbo ambazo anapenda kuzisikiliza akiwa mapumziko lakini pia mazoezini.