Mchungaji Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Centre amezua mjadala baada ya kudai kwamba muundo fulani wa tsheti unaweza kuharibu ndoa na mahusiano.
Pasta Ezekiel katika klipu moja ya video ambayo imesambaa mitandaoni alionekana akimtabiria nyota muumini mmoja katika ibada yake.
Muumini huyo alikuwa amevalia shati tao lenye nembo ya bendera ya Afrika kwa mbele, nembo ambayo Pasta Ezekiel alikemea vikali akisema kwamba ni nembo ya mikosi dhidi ya ndoa.
Kwa mujibu wa mchungaji huyo mwenye utata, tsheti zenye nembo kama hizo huwa zinazuia nyota ya ndoa kwa yeyote anayefanya uthubutu wa kuzivaa.
Mchungaji alimwambia kijana huyo asivae tena fulana hiyo akidai ni ya wataliki.
“Usivae tena kitambaa hiki. Yeyote anayevaa t-shirt hii hataolewa au kuoa. Ni kwa watu walioachwa tu. Usinunue nguo hiyo popote unapoikuta inauzwa. Najua wafanyabiashara watanichukia, lakini hakuna kitambaa ambacho hakina maana,” Mchungaji Odero alisema. Alieleza kuwa nguo zote zina umuhimu wa kiroho na huathiri hatima ya mvaaji.
Akitolea mfano, Pasta Ezekiel alisema kwamba rais mstaafu Uhuru Kenyatta alibadilisha mavazi yake pindi tu alipoingia ikuluni, akisema kwamba kuna baadhi ya mavazi mtu akivaa ni ishara ya kukaribisha mikosi maishani mwao.
“Kila kitambaa kina roho inayokufanya uvutiwe nacho. Kumbuka kabla Uhuru Kenyatta hajawa rais alikuwa amevaa vazi lolote, lakini alipokuwa rais, aliambiwa avae suti za bluu na tai nyekundu. Hiyo tai nyekundu ina maana ya uongozi,” alisema.