Madee aachia wimbo tata 'Nakojoa Pazuri' mamlaka zacharuka na kumpiga faini kubwa

“…na amepigwa faini ya shilingi milioni 3 kwa kosa hilo na kutofanya shughuli za Sanaa mpaka hapo atakapolipa faini husika,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Muhtasari

• Wiki chache zilizopita, pigo kama hilo liliwakuta wasanii Mbosso, Billnass na Whozu baada ya video ya wimbo wao wa Ameyatimba Remix kutajwa kuenda kinyume na maadili.

MADEE
MADEE
Image: X

Gwiji wa muziki wa Bongo Fleva, Hamad Alli Seneda, maarufu kama Madee amechokoza nyuki baada ya kuachia wimbo wenye mada tata ya ‘Nakojoa Pazuri’.

Msanii huyo baada ya kuachia wimbo huo siku chache zilizopita, mamlaka ya Sanaa nchini Tanzania, BASATA imemcharukia na kumpiga faini ya shilingi milioni 3 za kitanzania kwa kile wanasema ni mada ya kupotosha jamii.

“Mnamo Desemba 13, 2023, mwanamuziki anayejulikana kwa jina la kisanii kama Madee alichapisha wimbo wenye maudhui yanayokiuka kanuni za BASATA za 2018 na mwongozo wa uzingatiaji maadili katika kazi za Sanaa ya mwaka 2023. Baada ya kujiridhisha kuwa msanii huyo amefanya makusudi, Baraza imefikia maamuzi ya kumtaka msanii Madee kushusha wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, kuufunga wimbo kutokuimbwa na kuchezwa mahali popote ikiwemo kwenye vyombo vya habari…”

“…na amepigwa faini ya shilingi milioni 3 kwa kosa hilo na kutofanya shughuli za Sanaa mpaka hapo atakapolipa faini husika,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Pia produsa aliyezalisha wimbo huo hajaachwa nyuma kwani naye amekutwa na faini zito kwa kukubali kufanya wimbo ambao ni Dhahiri maudhui yake ni kinyume cha sheria.

“Producer ambaye anatambulika kwa jina la kisanii Mr T Touch anetozwa faini ya shilingi milioni 1 na pia mhusika aliyepandisha wimbo huo kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali ametozwa faini ya shilingi milioni 1,” taarifa hiyo ilisoma.

Wiki chache zilizopita, pigo kama hilo liliwakuta wasanii Mbosso, Billnass na Whozu baada ya video ya wimbo wao wa Ameyatimba Remix kutajwa kuenda kinyume na maadili kwa kuonesha mwanamke aliyekuwa akidhalilishwa kingono.