Msanii aliyeelewa na kukuzwa na Mdau wa Sanaa ya muziki wa Bongo Fleva, Mkubwa Fella, Aslay Isihaka hatimaye amejibu kauli ambayo meneja huyo wa Wasafi alitoa katika redio ya Wasafi FM kuhusu Aslay kusainiwa.
Awali tuliripoti kwamba Mkubwa Fella wakati wa mahojiano, alisema kwamba yeye kama meneja wa WCB Wasafi anafahamu kwamba kuna mipango kabambe ambayo inaendelea kupikwa kuona kwamba Aslay naye anakuwa mmoja wa wasanii chini ya lebo hiyo kubwa Afrika Mashariki.
Mkubwa alisema kwamba kwa sasa yuko kwenye mazungumzo endelevu na Diamond kuhakikisha kwamba Aslay naye anamfuata mwenzake, Mbosso ambaye walikuwa pamoja katika kundi la Yamoto Bend lililosimamiwa na Fella.
“Wakati Mbosso aliondoka Yamoto kujiunga na WCB Wasafi, nilitoa Baraka zangu zote na Diamond ndiye alikuwa mstari wa mbele kumpokea. Na ndio sasa hivi nafanya mpango naongea na Naseeb [Diamond] Mungu akijaalia yule Aslay ampe shavu kidogo, ni kijana ana talanta kubwa sana,” Mkubwa Fella alifichua.
Akijibu kauli hiyo, Aslay alionesha nia na ari ya dhati ya kutekeleza kile ambacho baba wake katika Sanaa ameona na kusema kwamba yuko tayari wenda kokote kule ambako Fella ataona atanufaika.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba kwa sasa yuko chini ya lebo ya Rockstar inayosimamiwa na Sony na kwa hivyo asingeweza kuzungumza sana.
“Sijawahi fanya mazungumzo yoyote ya kutaka kusainiwa WCB Wasafi, lakini yule ni Mkubwa, lazima nikubali kile anachosema. Ninatamani tu sehemu yoyote yaani sio tu WCB Wasafi bali sehemu yoyote tu ambayo ninaona kuna muongozo mzuri, mimi nitaenda. Lakini mnajua kabisa sasa hivi nipo kwenye rekodi lebo,” Aslay alisema.
Hii si mara ya kwanza kwa msanii huyo kujitokeza kubisha vikali kauli za kumhusisha na Wasafi, lakini pia itakumbukwa kwamba aliwahi weka wazi kuhusu uwezekano wa kufanya kolabo na Diamond kama nafasi itatokea.
“Diamond ni mtu mkubwa, ana uwezo wa kufanya kitu chochote na kwa wakati wowote na kikawa kikubwa. Kwa hiyo kutamani kunisaini WCB kwa sasa hivi hapana. Tayari nina malengo yangu na nina vitu vyangu ninavyotarajia kuvifanya. Lakini sijawahi fuatwa na Diamond kwamba anataka kunisaini wala watu wake hawajawahi nifuata,” alisema kwa wakati mmoja katika mahojiano na Millard Ayo mwezi Septemba.