Katika wiki za hivi karibuni, kumekuwa na mjadala pevu katika mitandao ya kijamii kuhusu mchango wa muasisi wa ucheshi wa kisasa nchini, Daniel Churchill katika kukuza wachekeshaji wengine na jinsi aliwakimu kimaisha.
Mjadala huu umejikita katika pande mbili tofauti, baadhi wakimsuta kuwa alikuwa anawatumia wachekeshaji chipukizi kujinufaisha huku wengine wakimvisha koja la maua kwa kufanya kazi kubwa kuwainua makumi ya wachekeshaji ambao wanajitegemea katika fani mbalimbali kwa sasa.
Mjadala huu ulichukua mkondo mwingine baada ya aliyekuwa mchekeshaji wa Churchill Show, YY Comedian kukiri kwamba Churchill kwa wakati mmoja alikuwa anawapa wachekeshaji wake kuchagua kati ya kupewa gari au laki 3 taslimu ili kujikimu.
Akionekana kumjibu, mchekeshaji mwenzake, MCA Tricky alisema kwamba Churchill hawezi kuangaliwa tu katika hilo pekee bali aliwapa wengi jukwaa la kujinadi na akajitolea mfano yeye kwamba kila kitu ambacho ako nacho sasa hivi ikiwemo chapa yake ni kutokana na nafasi aliyopewa na Churchill ukwaani.
“Hebu tuwe wepesi wa kushukuru kwa kile Churchill alichotufanyia. Mungu alimtumia Churchill kunipa magari, viwanja, kazi ya redio. Chapa yangu ilijengwa kwenye jukwaa la Churchill,” MCA Tricky alisema.
Mchekeshaji huyo ambaye kwa sasa ni mtangazaji katika kituo kimoja cha redio humu nchini alisema wengi walikuwa wanakwenda tu na kukabidhiwa nafasi jukwaani ya kuchekesha pasi na kujua Churchill alikuwa amegharamika kiasi gani kufanikisha shoo hiyo.
Tricky alisisitiza kwamba kuna haja ya Churchill kupewa maua yake angali hai ili ayanuse mwenyewe.
“Sijui kafara alizokuwa anapitia. Sisi kazi ilikuwa kuingia kwa stage, kuua na kutoka. Acha tupee mzae heshima yake,” Tricky alisema.