Harmonize alinitumia beat ya 'Single Again' nifanye remix lakini sikutaka - Rayvanny

Rayvanny alikuwa akiwajibu watu waliomvimbia kuwa anadandia ngoma za wasanii chipukizi anaposikia ni kali na kuwashawishi wafanye remix.

Muhtasari

• Rayvanny na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana waliamua kuzika tofauti zao baada ya malumbano yaliyozidi miaka miwili.

• Wawili hao walikutana baada ya Harmonize kuridhia kumletea Rayvanny tuzo yake kutoka tamasha la AEUSA nchini Marekani.

Harmonize na Rayvanny
Harmonize na Rayvanny
Image: maktaba

Msanii wa kizazi kipya mmiliki wa lebo ya Next Level Music, Rayvanny amewasuta wale wanaomponda kwa kushiriki katika remix za nyimbo nyingi pendwa za vijana chipukizi.

Akitoa taarifa kwa umma kuhusu hilo kupitia instastory zake, Rayvanny alisema kuwa wale wanaosema anadakia tu kila wimbo mkubwa kufanya remix ni wapuuzi kwani anachokifanya ni kuwainua wasanii chipukizi katika Sanaa.

Msanii huyo alitolea mfano wa nyimbo kubwa ambazo angetaka kufanya remix zikiwemo Enjoy ya Juma Jux na Diamond lakini pia akaitaja Single Again ya Harmonize.

Akizungumzia Single Again kama wimbo mkubwa, Rayvanny alisema kwamba angetaka kufanya remix wala asingesubiri kwani hata Harmonize mwenyewe aliwahi mtumia beat kwa ajili ya kufanikisha remix hiyo.

“Kwa wote watu wapuuzi, huu ni upungufu wa kutanua mawazo, ningetaka kufanya nyimbo zilizo hit ningefanya ENJOY, ningefanya SINGLE AGAIN tena hadi nilitumiwa beat na mzee Konde [Harmonize] mwenyewe. Kwa hiyo ukiona nimefanya wimbo basi jua nimeamua kufanya tu,” alisema.

Rayvanny alisema kwamba wanaomsema kuwa anasubiri wimbo mkali ndio anaudandia kufanay remix watamfanya akome kuwashirikisha wasanii chipukizi.

Pia alisema wakati anafanay remix na ngoma za wasanii wa nje, moja kwa moja si kudandia bali ni kulipwa amelipwa pesa ndefu.

“Msifanye nianze kukataa kufanya nyimbo na vijana wenzangu wakiomba tufanye kazi, usichokijua ukiona nimefanya remix ya nje jua nimelipwa tena hela nyingi,” alisema.

Rayvanny na Harmonize mwishoni mwa mwaka jana waliamua kuzika tofauti zao baada ya malumbano yaliyozidi miaka miwili.

Wawili hao walikutana baada ya Harmonize kuridhia kumletea Rayvanny tuzo yake kutoka tamasha la AEUSA nchini Marekani.

Rayvanny aliifuata tuzo hiyo kaitka Konde Village na pamoja wakazungumza kwa bashasha, Harmonize akisema aliamua kuzika uhasama kwa vile wote wameshakua sasa na haina haja wanao kuja kuishi wakijua kwamba baba zao ni maadui bila chanzo.