Babu Owino kuachia wimbo wake wa kolabo na Stevo Simple Boy

"Yuko katika tasnia ya utengenezaji wa Juisi ya Freshi Barida inayozalishwa kwa ladha tofauti. Tukuze Simple Boy,” Babu alisema.

Muhtasari

• Mbunge huyo mcheshi na mchapakazi pia aliendelea kusema kwamba hivi karibuni watafanya kolabo ya nguvu na msanii huyo.

Babu Owino na Stevo Simple Boy
Babu Owino na Stevo Simple Boy
Image: Facebook

Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino amekutana na rapa matata Stevo Simple Boy na kusema walifanya mazungumzo ya kina ambayo yataleta tija kwa maisha ya msanii huyo siku za hivi karibuni.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Babu Owino alipakia picha wakiwa na Stevo Simple Boy na kusema kwamba walikutana kwa maongezi ya kibiashara ambayo bila shaka waliyapatia ufumbuzi mkubwa.

Owino alisema atajitupa nyuma ya tevo Simple Boy kumuunga mkono katika kufanikisha ndoto yake ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha sharubati za ‘Freshi Barida’ – ndoto ambayo Stevo amekuwa akiidokeza tangu mwaka juzi walipoachana na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy.

“Nilifanya mkutano mzuri na Stevo Simple Boy. Yuko katika tasnia ya utengenezaji wa Juisi ya Freshi Barida inayozalishwa kwa ladha tofauti. Tukuze Simple Boy,” Babu Owino alisema.

Mbunge huyo mcheshi na mchapakazi pia aliendelea kusema kwamba hivi karibuni watafanya kolabo ya nguvu na msanii huyo na kuahidi mashabiki wake kuwa wimbo utatoka muda si mrefu.

“Pia tutafanya kazi pamoja katika tasnia ya muziki na kolabo itatoka hivi karibuni,” aliongeza.

Mashabiki wake walimpongeza kwa kuamua kumshika rapa huyo ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikiri kutofaidika pakubwa kutokana na kazi zake za muziki licha ya kazi hizo kupendwa na mashabiki wengi.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro alitoa maoni kwenye chapisho hilo akimhongera kwa kumshika Stevo mkono na kumtaka kuendelea na moyo huo.

“Hii ni nzuri Bro. Endelea kukuza werevu na bidii ya Hustlers. Naona ni kama uko karibu kuingia chama tawala,” Nyoro alimwambia.

“Bro napenda pia unavyofanya kazi pale Kiharu kwenye Elimu,” Owino alimjibu.