'Hii kanisa kama huleti sukari na majani nitakufukuza' - Pasta Kanyari awaonya waumini (video)

Mchungaji huyo pia alionekana kukasirishwa na kitendo cha waumini wake kwenda kumuona wakiwa na sadaka ya kati ya shilingi 200 hadi 500, akisema kwamba atawafukuza.

Muhtasari

• "Kama mimi ni baba yako hufai kuja kuniona mikono mitupu, nitakufukuza huku hautakaa,” Kanyari alihubiri katika video hiyo.

Pastor Kanyari
Pastor Kanyari

Video mpya imeibuka mitandaoni ikimuonhesha mchungaji mwenye utata, Victor Kanyari akiwatishia waumini wake ambao wanakwenda kanisani mikono mitupu.

Katika video hiyo, Kanyari alionekana akihubiri kuhusu waumini ambao wanamchukulia kama baba wao wa Imani lakini wanamwendea mikono mitupu, na kuapa kukomesha tabia hiyo.

Kanyari ambaye si mgeni kwa habari na mahubiri yenye ukakasi na utata alisema kwamba kuanzia kipindi cha mahubiri hayo ambayo hayajulikani ni ya lini haswa, hangeruhusu muumini yeyote anayekwenda kuhudhuria ibada pasi na kumpelekea bidhaa za kula kama vile sukari na majani miongoni mwa vingine.

Mchungaji huyo aliyeonekana kuwa na hasira akihubiri alisema kwamba pia asingependa kupelekewa shilingi 200 au 500 za kula, akiapa kuwafukuza watakaokaidi amri zake mpya kama kweli wanamchukulia kama baba wao wa kiroho.

“Hii kanisa kama utakuwa hukuji na sukari na majani na unaniletea shilingi 200 au 500 za kula nitakufukuza… mimi kama ni baba yako huwezi kuwa unakuja kuniona mikono mitupu, sitakubali. Kama mimi ni baba yako hufai kuja kuniona mikono mitupu, nitakufukuza huku hautakaa,” Kanyari alihubiri katika video hiyo.

Mchungaji huyo mwenye ukakamavu wa aina yake licha ya kukashifiwa vikali amekuwa kweney vichwa vya habari siku za nyuma alipotumbuliwa na njama zake za kuwatoza waumini sadaka maarufu 310.

Katika ufichuzi uliofanywa na mbunge wa Nyali Mohammed Ali kipindi hicho akiwa mwanahabari, makumi ya watu walijitokeza na kukiri jinsi mchungaji huyo alikuwa anawahadaa kwa kuwalipa ili kuigiza kanisani kwamba amewaombea na kupata miujiza.

Licha ya ufichuzi huo kumpaka tope Kanyari, alizama kwa muda lakini akaibukia na kanisa lingine na amekuwa akiendelelza ibada zake za mahubiri kwenye runinga na ukweli usemwe, bado ana wafuasi wengi tu ambao wanamtii na kumuona kama baba wa kiroho – ila sasa tatizo ni kwamba wanamwendea mikono mitupu, jamboambalo linaonekana haliko sawa kwa upande wake.