Msanii Brown Mauzo amemsherehekea mama yake mzazi kwa njia ya kipekee kwa kupakia picha yao ya zamani kabla hajatusua kimuziki.
Mauzo kupitia kwa Instagram story yake alichapisha picha kutoka kwa TikTok yake ikimuonyesha amekumbatiana na mamake na kusema kwamba mama ndiye mwanamke pekee ambaye kamwe hawezi kutoa moyoni mwake.
Baba huyo wa watoto wawili na mwanasosholaiti Vera Sidika alisema kwamba hakuna mwanamke mwingine duniani anayeweza kuifikia nafasi ya mama katika maisha ya mtu, kwani huyo ndiye mwanamke pekee ambaye ana uwezo wa kukubeba tumboni miezi tisa, mikononi miaka mitatu ya malezi lakini pia kukuhifadhi moyoni milele.
“Mama ndiye kiumbe pekee ambaye anaweza kukubeba tumboni miezi 9, kukupakata mikononi miaka 3 na kukuhifadhi daima katika moyo wake, nakupenda sana mamangu,” Brown Mauzo aliandika kwenye picha hiyo ya TBT.
Mauzo anasema haya baada ya penzi lake na Vera Sidika kufikia kikomo mwaka jana.
Licha ya kumpa hakikisho mara kwa mara kwamba asingemuacha, Vera Sidika alivunja nadhiri hiyo na kumtema Mauzo Agosti baada ya kuzaa pamoja watoto wawili.
Kwa sasa, wawili hao wanashirikiana tu kwa malezi ya wanao, kila mmoja akionekana kukubali kusonga mbele na maisha yake.