'KCSE ukipata D usirudi Jacaranda', Okanga aambiwa, apewa kalamu 200 kuingia form 1

“Hizi kalamu kuna vile utazitumia, kidato cha kwanza utatumia kalamu 20, kidato cha pili utatumia kalamu 50, kidato cha tatu utatumia kalamu 70…" Okanga aliambiwa.

Muhtasari

• "Nuru Okanga tunakuambia, venye unaenda kidato cha kwanza, ukirudi na D…” alielekezwa.

Nuru Okanga aandaliwa kwenda form 1
Nuru Okanga aandaliwa kwenda form 1
Image: Facebook//screengrab.

Nuru Okanga amefanyiwa tafrija ya kumuaga kutoka kwa Bunge la Wananchi ili kumruhusu kujiunga na kidato cha kwanza.

Hafla hiyo iliyofanyika katika uwanja wa Jacaranda, ambapo huwa wanafanyia mkutano wa Bunge la Wananchi uliandaliwa na marafiki zake wa karibu ambao walimnunulia baadhi ya zawadi ili kuingia sekondari.

Akikabidhiwa vitu hivyo ambavyo vilijumuisha kalamu na vitabu, walimtania kwamba akienda baada ya miaka 4 aanguke mtihani wa kufuzu sekondari, KCSE basi moja kwa moja watampiga marufuku kuhudhuria mikutano yao Jacaranda.

“Tuko na mtahiniwa wetu, mwenye anaenda kidato cha kwanza, na hapa tumemnunulia kalamu, anataka pia vitabu. Nuru usirudi hapa ukipata D,” walimtania huku wakimkabidhi

 Wakiendelea kumpa, walimpa pia maagizo ya jinsi atatumia kalamu hizo zote kwa uadilifu na kama atazingatia maagizo hayo, basi miaka yote minne huneda hatonunua kalamu nyingine tena

“Hizi kalamu kuna vile utazitumia, kidato cha kwanza utatumia kalamu 20, kidato cha pili utatumia kalamu 50, kidato cha tatu utatumia kalamu 70…Nuru Okanga tunakuambia, venye unaenda kidato cha kwanza, ukirudi na D…” alielekezwa.

Jamaa huyo aliyekuwa akimpa maelekezo alimsifia Okanga kuwa ni mtu aliyevunja rekodi Kenya nzima kwa kufanya mtihani wa KCPE japo hakuweza kutaja alama alizopata, wandani wake wameendelea kusisitiza kwamba alivuka alama Zaidi ya 400.

Pia walimtania kwamba anapoenda shule, watafanya mazungumzo na mwalimu mkuu ili aruhusiwe kutovaa sare na badala yake kuvaa suti yake.

Walimtaka kuwaelezea walimu mapema siku ya maandamano kwamba hatohudhuria masomo siku hiyo.

Okanga ni mmoja wa watetezi wakali wa sera za kiongozi wa ODM, Raila Odinga na alisema katika mahojiano na Radio Jambo kwamba sababu kuu iliyomchochea kurudi shule ni kujiandaa kwa ajili ya kuwania kama MCA katika wadi ya Kholera uchaguzi ujao.

Okanga alisema kwamba asingependa kuja kuwa kiongozi ambaye hana vyeti vyovyote vya kuonesha elimu yake.