Mr Nice: Nikifa leo hii watu wataendelea kumuona Mr Nice kupitia kwa Diamond Platnumz

Muhtasari

• “Enzi zangu ilikuwa kawaida kukodiwa private jet kwenda kwenye shoo. Ilikuwa kawaida sana kwangu kupanda ndege ya peke yangu," alisema.

Diamond na Mr NIce
Diamond na Mr NIce
Image: Facebook, Screengrab

Mkongwe wa Bongo Fleva, Mr Nice amemsifia pakubwa msanii anayeteka anga kwa sasa Diamond Platnumz na kufichua kwamba msanii huyo ndiye anayebeba uhalisia wake wa zamani enzi zake.

Nice kupitia kipindi cha Jana na Leo kwenye stesheni ya Wasafi alisema kwamba hata akifa leo hii mashabiki wake hawatomkosa kwani watakuwa wanamuona kwa vitendo vyake kimuziki kupitia msanii Diamond Platnumz.

Mr Nice alisema kwamba kila kitu ambacho anafanya Diamond sasa hivi kuanzia mavazi, kuruka na ndege ya kibinafsi kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila kusahau kuvuma ndani na nje ya Tanzania, ndio picha halisi ya yeye enzi zake.

“Enzi zangu ilikuwa kawaida kukodiwa private jet kwenda kwenye shoo. Ilikuwa kawaida sana kwangu kupanda ndege ya peke yangu, Marekani kwangu ilikuwa kama ziara ya kwenda sokoni na kurudi. Ndio vitu anavyofanya Diamond sasa hivi, yaani nakwambia mimi nikifa bado Mr Nice ataendelea kuwepo kupitia Diamond,” Mr Nice alisema.

Alimtetea Diamond kwa kuonesh maisha yake mitandaoni akiruka kutoka sehemu moja kwenda nyingine na ndege ya peke yake, akisema kwamba mtu akiwa msanii mkubwa kuna vitu lazima tu avifanye kudhihirisha ukubwa wake.

“Watu wanasema ooh eti sijui Diamond anajifanya… hajifanyi! Huo ndio wakati wake uko hapo na hayo mambo yanawezekana sio kwamba anaigiza, ni kwa sababu huu ndio muda wake. Wewe kata au kubali, Diamond ndiye yuko kwa sasa hivi, utafanyaje? Labda ukajinyonge,” alisema.

Msanii huyo alijitapa kwamba enzi zake alikuwa na pesa nyingi mpaka zingine alikuwa anabeba kwenye buti la gari lake, kwani kwake ilikuwa ji jambo la kawaida kuona pesa.

“Hiyo ilikuwa ni kawaida, hivyo vitu vipo vina wakati wake na vinapita. sasa hivi mkiniambia nifanye hivyo vitu siwezi kwa sababu umri nao umekwenda na mazingira nayo yamebadilika,” aliongeza.

Mr Nice alisema japo ndoto yake ni kutaka kufanya kolabo na msanii yeyote kati ya wengi wa kizazi kipya ambao wameibukia, ila angependa sana kufanya kolabo na Diamond Platnumz.