Mpenzi mpya wa Manzi wa Kibera afichua kilochomchochea kumpenda sosholaiti huyo

Mzee Njau alisema kwamba mipango ya harusi yao itafanyika na kukiri kwamba hivi karibuni ataongozana na Manzi wa Kibera kwenda kujitambulisha kwa wazazi wake.

Muhtasari

• Mzee huyo pia alifutilia mbali uwezekano wowote wa kuachwa siku moja na sosholaiti huyo.

• “Sina shaka na hilo, mimi sina hiyo habari kwamba ataniacha, labda yeye aniache tu, sioni ikifanyika." alisema.

Manzi wa KIbera na mzee wake wa miaka 75
Manzi wa KIbera na mzee wake wa miaka 75
Image: Screengrab

Daniel Njau, mzee wa miaka 75 ambaye ni mpenzi mpya wa mwanasosholaiti Manzi wa Kibera kwa mara ya kwanza amefunguka kwa undani kilichomchochea kumpenda sosholaiti huyo wa kutoka mitaa ya mabanda ya Kibera.

Ikiwa ni wiki tatu tangu Manzi wa Kibera amtambulishe kama mpenzi wake mpya, wawili hao wameketi na YouTuber Nicholas Kioko na Njau aliweza kufichua vitu ambavyo vilimvutia kwa mrembo huyo.

Kwa mujibu wa mzee huyo, ilimchukua muda mrefu sana kumchunguza na kumfuatilia mienedo yake na mpaka kuridhika kwamba anamfaa kabla ya kukubali kutambulishwa hadharani.

“Lile jambo lilinifanya nimpende, ni kuona yeye ni mkamilifu kwa kila jambo, tabia zake pia zilinifurahisha, watu anaotembea nao pia walinifurahisha, maana yeye haendi na haya makundi ya kuvuta sigara, dawa za kulevya nini, yeye ni mtulivu. Na ilinichukua muda kumuangalia mienendo yake nikaona huyu ananifaa,” Mzee Njau alisema kwa ujasiri.

Mzee huyo pia alifutilia mbali uwezekano wowote wa kuachwa siku moja na sosholaiti huyo ambaye tunaweza tukasema ana hulka ya kupenda na kuacha pasi na nukta ya haya.

“Sina shaka na hilo, mimi sina hiyo habari kwamba ataniacha, labda yeye aniache tu, sioni ikifanyika. Vile ambavyo tumeishi kwa siku chache, sioni hizo dalili na sidhani,” alisema

Kwa upande wake, Manzi wa Kibera pia aligonga kwenye mshono akisema kwamba hadhani kama atawahi kuja kumuacha mzee huyo kwani ameshafika mwisho na kituo amekitia.

“Sidhani, sioni kama itatokea, nimefika sasa mwisho.”

Kwa swali la kizushi kuhusu hali yake ya akili, mzee huyo alisema kwamba wengi wanamuona kama tahahira lakini ukweli ni kwamba yeye yuko sawa kabisa wala hatumii dawa za kulevya wala vilevi.

“Niko sawa kabisa mimi, situmii hata dawa zozote. Niko timamu kiafya, na kiakili pia, kimawazo nawaza vyema. Hata kichwa hakiniumi, hata stress sina,” Mzee huyo alihakiki.

Mzee Njau alisema kwamba mipango ya harusi yao itafanyika na kukiri kwamba hivi karibuni ataongozana na Manzi wa Kibera kwenda kujitambulisha kwa wazazi wake.